8 C
New York

Mwangwi wa sheria| Polisi haihusiki na kesi hizi

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

WAKATI mwingine, kutokujua sehemu sahihi ya kupeleka malalamiko yako kunaweza kukupotezea muda, nguvu, na hata haki yako.

Mathalan, kwenda polisi kwa suala la madai ni kosa ambalo limekuwa likifanywa na walalamikaji wengi, bila kufahamu kuwa chombo hicho kinashughulika na makosa ya  jinai tu.

GAZETINI imefanya mahojiano na Wakili Baraka Asajile Gwakabake, ambaye anafafanua kwa kina namna kesi za madai zinavyoshughulikiwa, mahali sahihi ya kupeleka malalamiko na sheria zinazohukumu.

Wakili huyo anaanza kwa kusema Sheria za kesi za madai hazifanyi kazi kwa jazba, bali kwa kufuata utaratibu. Madai yanahitaji uthibitisho, nyaraka, na mamlaka sahihi ya kisheria.

Kwa mujibu wake, Polisi wanalinda maslahi ya jinai, si kugawa ardhi, si kulazimisha deni, si kupima mchango wa ndoa, wala si kuamua mirathi.

“Ukichanganya mamlaka, unajitengenezea vikwazo mwenyewe. Utaratibu sahihi si anasa, si upendeleo, wala si kuchelewesha haki.

“Mahakama ipo kusikiliza, kupima, na kuamua kwa haki. Hapo ndipo madai yanapata thamani yake halisi,” anasema Wakili Baraka kuiambia Gazetini.

Je, kwa mujibu wa wakili Baraka, ni kesi zipi zenye msingi wa madai, ambazo mlalamikaji hapaswi kukimbilia polisi?

Migogoro ya ardhi na viwanja

Hapa kinachoamuliwa ni umiliki, mipaka, au haki ya matumizi. Ni suala la nyaraka, ramani, ushahidi wa umiliki. Anasema: “Polisi hawagawanyi ardhi wala kuamua nani ni mmiliki halali.

“Mahali pa kwenda ni Baraza la Ardhi la Kata, Baraza la Ardhi la Wilaya, au Mahakama ya Ardhi kulingana na thamani na hatua ya shauri. Sheria zinazotumika hapa ni Sheria ya Ardhi na Sheria ya Ardhi ya Vijiji.

“Hapa kinachotazamwa ni umiliki halali, mipaka, na haki ya matumizi. Polisi hawana mamlaka ya kugawa au kufuta umiliki.”

Migogoro, mali za ndoa

Mgawanyo wa mali, madai ya mchango wa mke au mume, au haki baada ya kutengana. Ni madai ya haki na usawa.

Wakili Baraka anasema: “Polisi hawapimi mchango wa kupika, kulea watoto, au kushiriki ujenzi. Mahali pa kwenda ni Bodi ya Usuluhishi wa Ndoa, Mahakama ya Mwanzo au Mahakama ya Wilaya. “Sheria inayotumika ni Sheria ya Ndoa. Mgawanyo wa mali, mchango wa wanandoa, na haki baada ya kutengana ni masuala ya madai, si jinai.”

Itaendelea…

Mawasiliano: Wakili Baraka Asajile Gwakabake – 0784745645

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img