8.8 C
New York

Nicola Peltz; Mkwe anayeivuruga familia ya Beckham

Published:

LOS ANGELES, Marekani

Kwa sasa, mtoto wa kiume wa Beckham, Brooklyn, haongei na baba wala mama yake. Kama hiyo haitoshi, alishahama nyumbani kwao na kujiweka mbali na familia yake hiyo.

Kwanini? Taarifa za awali za vyombo vya habari zilidai kuwa hakukuwa na maelewano mazuri kati ya Nicola na mama mkwe wake, Victoria.

Aidha, ikaelezwa kuwa hata baba mkwe, Beckham, naye hakuwa akipendezwa na kitendo cha Brooklyn kuwa na Nicola. Hiyo kwa mujibu wa vyombo vya habari.

Sasa, hivi karibuni Brooklyn ameibuka na kuwafyatulia maneno makali wazazi wake akisema hawajawahi kumpenda mkewe.

Kwamba hata wakati wakiishi pamoja, mama yake alifikia hatua ya kuwaalika wasichana wengine nyumbani li tu kumkera Nicola.

Kwa ufupi, Brooklyn anaamini mama yake, Victoria, hajawahi kumpenda Nicola na amekuwa akimvunjia heshima.

Hajaishia kwa mama tu, bali Brooklyn amemvaa hata baba yake, Beckham, akidai kuwa aliwahi kumwambia kuwa hawezi kukaa naye meza moja akiwa na Nicola.

Brooklyn anawashutumu wazazi wake akiwataja kufanya jitihada kubwa za kuhakikisha ndoa yake na Nicola inavunjika.

“Nimekuwa kimya kwa miaka mingi, nimejaribu sana kulifanya jambo hili kubaki kuwa siri. Kwa bahati mbaya, wazazi wangu na watu wao wameendelea kwenda kwenye vyombo vya habari.

“Hivyo basi, kwa sasa sina mpango wa kupatana na familia. Sitawaliwi tena. Kwa mara ya kwanza, nasimama peke yangu,” amesema Brooklyn mwenye umri wa miaka 26.

Kijana huyo amedai kuwa kitendo cha kumuoa Nicola ndiyo sababu ya uhusiano mbaya uliopo kati yake na wazazi wake.

Lakini, chanzo cha ugomvi wa Victoria na Nicola kinatajwa na vyanzo vya habari kuwa ni gauni la harusi. Kwamba Nicola alikataa kuvaa gauni alilobuni mama mkwe wake wakati wa harusi mwaka 2022.

Katika hatua nyingine, mtoto mwingine wa kiume wa Beckham, Romeo, anatajwa kuwa chanzo cha ugomvi. Kivipi?

Inasemekana kuwa Brooklyn hakufurahia kitendo cha Romeo kutoka kimapenzi na mrembo Kim Turnbull. Taarifa zinaeleza kuwa Kim, ambaye ni ‘Dj’ maarufu jijini London, aliwahi kuwa na uhusiano na Brooklyn.

Akijibu hilo, Brooklyn anamkingia kifua mkewe akidai kuwa kitendo cha gauni hilo kutokuvaliwa ni uamuzi wa Victoria na si Nicola.

Mara ya mwisho kwa Brooklyn kujumuhika na familia yake, kwa maana ya wazazi na wadogo zake watatu (Romeo, Cruz na Harper) ilikuwa wakati wa Sikukuu ya Krismas mwaka 2024.

Mei, mwaka jana, iliwashitua wengi baada ya Brooklyn kutokuonekana katika sherehe ya kumbukizi ya siku ya kuzaliwa (birthday) ya baba yake, Beckham.

Na badala yake, wiki chache baadaye Brooklyn alimtumia ujumbe wa kumtaki kheri baba mkwe wake, Nelson Peltz, ambaye naye alikuwa akisherehekea ‘birthday’ yake.

Ikumbukwe, hata Brooklyn na Nicola walipokuwa wakifanya kumbukizi ya ndoa yao, hakuna mwanafamilia wa Beckham hata mmoja aliyehudhuria.

Kama hiyo haitoshi, hakuna ‘anayem-follow’ mwenzake katika mitandao ya kijamii. Uadui huo wa mitandaoni upo pia kati ya Brooklyn na wadogo zake; Romeo, Cruz na Harper.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img