Na mwandishi wetu, Gazetini
UHUSIANO wa Marekani na Afrika Kusini umezidi kudorora kwa siku za hivi karibuni na tayari Rais Donald Trump ametaka nchi hiyo kuondoshwa katika Umoja wa G20 (mataifa tajiri 20 duniani).
Ikumbukwe, ni miezi mitatu tu imepita tangu Rais Trump na Serikali yake walipotangazia Afrika Kusini ongezeko la ushuru wa asilimia 30 kwa bidhaa zake zinazoingia nchini humo.
Sasa, Rais Trump anataka Afrika Kusini isiwe sehemu ya G20 zikiwa zimebaki siku chache kuelekea Mkutano Mkuu wa Umoja huo wa nchi zenye uchumi mkubwa unaotarajiwa kufanyika jijini Johannesburg.
Kutokana na kile anachodai kuwa Afrika Kusini imekuwa ikiwatesa watu weupe nchini humo, Rais Trump amegoma kuhudhuria Mkutano huo na badala yake atamtuma mwakilishi, ambaye ni Makamu wa Rais, JD Vance.
“Afrika Kusini haipaswi kuwa sehemu ya G20 kwa sababu kile kinachoendelea ni kibaya sana. Sitokuwepo kuwakilisha nchi yangu. (Mkutano) haukupaswa kufanyika pale,” amesema.
Hata hivyo, Afrika Kusini imeendelea kukanusha madai ya Rais Trump, pia takwimu za uhalifu hazioneshi kuwa watu weupe (wazungu) ni wahanga wakubwa wa matukio ya uhalifu nchini humo.
Afrika Kusini inaweza kuondoshwa G20? Umoja huo ulianzishwa mwaka 1999 na nchi wanachama ni zile zenye asilimia zaidi ya 85 ya utajiri wa dunia.
Tangu Mkutano wa kwanza uliofanyika mwaka 2008, marais wa nchi hizo wamekuwa wakikutana kila mwaka na kujadili changamoto zinazozikabili nchi hizo, pamoja na hali ya uchumi wa dunia.
Hakuna utaratibu rasmi wa nchi kuondoshwa G20 kwa sababu hakuna mkataba iliosaini wakati wa kujiunga, ni tofauti na ilivyo kwa jumuhiya zingine, ikiwamo Umoja wa Mataifa.
“Endapo nchi itatolewa G20, itamaanisha tu kwamba haitakuwa imealikwa kushiriki mkutano husika,” anasema Dkt. Andrew Gawthorpe wa Kituo cha Sera cha Kimataifa nchini Uingereza.
Lakini, kwa mujibu wa Dkt. Gawthorpe, uamuzi wa nchi kutokualikwa katika Mkutano unapaswa kupitishwa na wanachama wote wa G20.
Kwa upande mwingine, wachambuzi wa siasa barani Afrika hawaoni uwezekano wa Rais Trump kufanikiwa kuitenga Afrika Kusini na G20.
Kwa upande wake, mchambuzi Chris Vandome anaitolea mfano Urusi, akisema licha ya tishio la kuondoshwa G20 baada ya kuivamia Ukraine mwaka 2022, bado imeendelea kuwa sehemu ya Umoja huo.
Published:


