12.5 C
New York

Nini chanzo idadi ndogo ya wapiga kura?

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini
LICHA ya Rais Alassane Ouattara kushinda na kurejea madarakani kwa muhula wa nne, idadi ndogo ya wananchi waliojitokeza kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu imewashitua wengi na kuzua mjadala mkubwa juu ya mwenendo wa demokrasia nchini Ivory Coast.
Ouattara, ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 14, ameshinda kiti cha urais kwa asilimia 89.77 ya kura kupitia Chama cha Rally of Houphouetists for Democracy and Peace (RHDP).
Hata hivyo, kati ya watu milioni tisa waliojiandikisha kupiga kura, ni milioni 4.5 pekee, sawa na asilimia 50, waliojitokeza kutumia haki hiyo ya Kikatiba.
Idadi hiyo ni ndogo zaidi kuwahi kutokea katika chaguzi za Ivory Coast, ikiwa ni chini ya asilimia 53 ya wapiga kura wa Uchaguzi uliopita wa mwaka 2020.
Swali ni je, kwanini idadi ya wapiga kura imepungua kwa kiasi hicho? Wachambuzi wa siasa wanaamini wananchi hawaridhishwi na mazingira ya ushindani, hasa katika nafasi ya urais.
Mathalan, kuelekea Uchaguzi wa mwaka huu, wagombea wenye nguvu kwa upande wa upinzani, akiwamo Rais wa zamani, Laurent Gbagbo, walizuiwa kugombea.
Pia, wananchi walio wengi ni kama wamekata tamaa na hawaoni tena namna boksi la kura linavyuoweza kubadili maisha yao. Ni kutokana na Serikali kushindwa kumaliza changamoto nyingi, zikiwamo za kiuchumi, zinazolikabili Taifa hilo.
Baadhi ya changamoto zinazotajwa kuwa ni sugu ni uhaba wa ajira kwa vijana, ubovu wa miundombinu, ubora usioridhisha wa huduma za jamii, pamoja na vitendo vya rushwa serikalini.
Kwa upande mwingine, kwa miaka ya hivi karibuni, chaguzi za Ivory Coast zimeshuhudia machafuko makubwa baada ya mshindi wa urais kutangazwa.
Mwaka 2010, watu 30,000 walifariki, wakati Uchaguzi uliopita wa mwaka 2020 ulishuhudia vifo 85. Kwa mwaka huu, watu sita walipoteza maisha wakati wa kampeni.
Nini hatima ya Uchaguzi wa mwaka huu? Katika baadhi ya maeneo, hata baada ya matokeo ya kutangazwa, yamekuwapo maandano ya kupinga Rais Outtara kurejea madarakani.
Licha ya Serikali kutishia kuwafungulia mashitaka, viongozi wa vyama vya upinzani wameendelea kusisitiza kutoutambua ushindi wake.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img