12.5 C
New York

Umoja wa Afrika na presha ya mapinduzi ya kijeshi

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini
MBALI ya kulaani tukio la jeshi kupindua Serikali, Umoja wa Afrika (AU) umesitisha kwa muda uanachama wa Madagascar, huku hatua hiyo ikikosolewa vikali na wachambuzi wa siasa.
AU, kama ilivyo kwa Umoja wa Mataifa (UN), ilieleza kutokuunga mkono kitendo cha jeshi kumpindua Rais Andry Rojaelina baada ya maandano ya vijana wa nchi hiyo yaliyodumu kwa wiki tatu.
Kiongozi wa jeshi, Kanali Michael Randrianirina, aliapishwa Ijumaa ya wiki hii kuwa Rais wa Madagascar na kusema hatua hiyo imetokana na kiu ya mabadiliko waliyonayo vijana wa Taifa hilo.
Madagascar inaungana na mataifa ya Sudan, Mali, Guinea, Burkina Faso, Niger na Gabon, ambayo pia AU iliyasitishia uanachama baada ya mapinduzi ya kijeshi.
Katika taarifa yake baada ya mkutano wa dharura wa kuijadili Madagascar, Mwenyekiti wa AU, Mahmoud Ali Youssouf, alisema: “Utawala wa sheria unapaswa kuwa juu ya utawala wa mabavu.”
Hata hivyo, wachambuzi wa siasa wanakosoa hatua ya AU kusistisha uanachama wa Madagascar wakisema hiyo imebaki kuwa njia pekee na si kutafuta suluhisho la matukio ya mapinduzi ya kijeshi.
Mchambuzi wa masuala ya usalama barani Afrika, Fidel Amakye Owusu, anaiona AU ikiwa imeshindwa kabisa kutafuta suluhisho la matukio ya aina hiyo, na badala yake kuishia kutoa adhabu tu.
Aidha, mtazamo wake hautofautiani na alionao Ryan Cummings, ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Signal Risk ya Afrika Kusini, anayeamini kuwa kusitisha uanachama imebaki kuwa njia pekee ya AU katika kushughulikia ukiukwaji wa demokrasia.
Kwa upande wake, Taasisi ya masuala ya usalama ya ISS yenye makao makuu yake nchini Afrika Kusini nayo inaungana na wasomi hao, Amakye Owusu na Cummings.
ISS inaenda mbali zaidi na kutolea mfano Sudan, Mali na Burkina Faso, ikisema adhabu ya kusitishiwa uanachama wa AU haijawa somo kwa mataifa mengine kuepuka mapinduzi ya kijeshi.
Wakosoaji wanasema Umoja huo umekuwa ukichelewa kuchukua hatua katika kushughulikia migogoro ya kisiasa iliyopo kwa wanachama wake.
Lakini, kwa baadhi ya wachambuzi, ni ngumu kwa AU kuingilia migogoro ya ndani. Moja ya misingi ya Umoja huo ni wanachama wake kuwa na mamlaka kamili, yaani kujiongoza bila kuingiliwa.
Kwamba AU imekuwa ikijaribu kutokuingila masuala ya ndani ya nchi, hadi pale itakapoombwa kufanya hivyo. “Iko wazi kwamba AU siyo mamlaka kamili inayoruhusiwa kuingilia moja kwa moja masuala ya ndani ya nchi. Kwa hali ilivyo sasa, nchi zina nguvu kubwa (kuliko AU),” anasema Owusu kuiambia DW.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img