Na mwandishi wetu, Gazetini
SIASA za Afrika Mashariki zimegubikwa na simanzi nzito baada ya kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Amolo Odinga. Mwanasiasa huyo amefariki akiwa na umri wa miaka 80.
Taarifa za kufariki kwake zilithibitishwa jana Oktoba 15, 2025, na Hospitali ya Devamatha iliyoko katika Jimbo la Kerala nchini India, ambako Odinga alikwenda kwa ajili ya matibabu. “Odinga alianguka ghafla kwa shambulio la moyo …” ilieleza taarifa ya Hospitali hiyo.
Kwa upande mwingine, Odinga ameondoka katika uso wa dunia akiwa hajatimiza ndoto yake kubwa ya kuwa rais wa Kenya. Alijaribu kugombea kiti hicho mara tano katika miaka 30 ya hivi karibuni. Hakufanikiwa kuingia Ikulu.
Wachambuzi wa siasa za Afrika Mashariki wanaamini kama kuna kipindi Odinga alikaribia zaidi kutimiza ndoto yake hiyo, basi ni katika Uchaguzi wa mwaka 2007.
Akiwa anakabiliana na Mwai Kibaki katika kinyang’anyiro cha urais, Odinga alivuna ushawishi mkubwa, hasa kutoka katika Kabila lake la Luo huko Magharibi mwa Kenya.
Ni kutokana na nguvu kubwa aliyokuwa nayo katika mikutano yake ya kampeni, wachambuzi wa siasa waliamini ni wakati wake kuingia Ikulu. Haikuwa hivyo.
Baada ya Tume kumtangaza Kibaki anayetokea Kabila jingine kubwa, Kikuyu, kwa ushindi wa asilimia 46 dhidi ya asilimia 44 za Odinga, matokeo hayo yalifuatiwa na machafuko. Kama itakumbukwa, yalikuwa ni machafuko yaliyohusisha zaidi makabila hayo.
Ingawa mamia ya watu walipoteza maisha, Odinga hakutajwa kuwa chanzo cha machafuko. Ni tofauti na William Ruto na Uhuru Kenyata, ambao wamewahi kushutumiwa kwa kuwa chanzo cha ghasia katika siasa za Kenya.
Ikumbukwe, Ruto na Kenyata walikuwa miongoni mwa watuhumiwa sita waliofunguliwa mashitaka na Mahakama ya Uhalifu wa Kivita ya Kimataifa (ICC) mwaka 2010. Mashitaka dhidi yao yaliondoshwa baadaye.
Odinga alitokea wapi? Alizaliwa Januari 7, 1945, mjini Kisumu. Ni mtoto wa aliyewahi kuwa Makamu wa Rais wa kwanza wa Kenya, Jaramogi Oginga Odinga.
Baada ya kumaliza masomo yake ya uhandisi nchini Ujerumani, Odinga alirejea Kenya katika miaka ya 1970 na kuajiriwa kufundisha Chuo Kikuu cha Nairobi.
Aidha, umaarufu wake katika siasa ulianza katika miaka ya 1980, wakati huo akiwa ni mwanaharakati wa kisiasa aliyekosoa utawala wa chama kimoja chini ya Rais Daniel arap Moi.
Mwaka 1982, jina la Odinga lilitajwa katika wale waliohusishwa na jaribio la kuipindua Serikali. Baba yake, Jaramogi, naye alihusishwa na mpango huo.
Akishitakiwa kwa kosa la uhaini, Odinga alisota gerezani kwa muda mrefu, kabla ya kukimbilia Ulaya baada ya kuachiwa mwaka 1991.
Aliporejea Kenya mwaka 1992, alichaguliwa kuwa mbunge wa upinzani mjini Nairobi. Miaka 20 ndani ya Bunge ilimpa jina kubwa katika siasa za Kenya kwa namna alivyokuwa akipaza sauti juu ya rushwa na umasikini.
Mwaka 1997, aliianza rasmi safari yake ya kuwania urais lakini hakufua dafu. Ndipo alipokubali kuwa Waziri wa Nishati katika Serikali ya Moi mwaka 2001.
Baadaye, mwaka 2002, alimuunga mkono Kibaki katika kuwania kiti cha urais. Ilipofika mwaka 2007, wawili hao wakawa wapinzani wakubwa kuiwania nafasi ya kwenda Ikulu, Uchaguzi uliosababisha machafuko kama ilivyoelezwa awali.
Mwaka 2017, ulikuwa ni Uchaguzi wake wa nne kuwania urais. Mara yake ya mwisho kugombea nafasi hiyo ni katika Uchaguzi wa mwaka 2022 uliomuweka madarakani Rais Ruto. Odinga alikuwa akiungwa mkono na Kenyatta.
Licha ya madai yake ya kuchezewa rafu, haikubadili matokeo. Licha ya kusaini makubaliano na Serikali ya Rais Ruto yaliyokipa Chama chake cha ODM nafasi ya kuhusika katika uaandaji wa sera, pia wanasiasa wake wakiteuliwa kuwa sehemu ya Baraza la Mawaziri, bado Odinga ameondoka akiwa hajatimiza ndoto ya kuingia Ikulu.
Published:


