Na mwandishi wetu, Gazetini
TUJIKUMBUSHE; Septemba 14, mwaka huu, Gazeti la Washington Post liliutangazia ulimwengu juu ya mazungumzo kati ya Marekani na Serikali inayoongozwa kijeshi nchini Mali.
Kwamba katika mazungumzo hayo, Marekani ilikuwa ikilenga kuisaidia Mali katika vita dhidi ya magaidi wa ndani wanaoitesa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Baada ya habari hiyo ya Washington Post, Afrika ilishuhudia viongozi waandamizi wa Marekani wakiingia Afrika na kukutana na wenzao wa Serikali ya Mali.
Kuanzia hapo, mataifa mawili hayo yamekuwa yakishirikiana bega kwa bega, huku Marekani ikitoa msaada mkubwa wa kijeshi kwa wenzao hao.
Lakini, licha ya kuonekana ni mpango wa kukabiliana na ugaidi, wachambuzi wa siasa za kimataifa wanaamini kuwa Marekani inapiga hesabu zingine tofauti.
Historia inakumbusha kuwa wakati kiongozi wa sasa wa Mali, Jenerali Assimi Goita, anafanya mapinduzi ya kijeshi miaka mitano iliyopita, Marekani haikuonesha nia ya kushirikiana naye.
Si tu haikutaka kushirikiana naye, bali pia Marekani ililaani mapinduzi hayo na hata kusitisha msaada wa masuala ya usalama kwa Taifa hilo.
Je, kwanini Marekani imesahau hayo na sasa inashirikiana Jenerali Goita, ambaye amejipa miaka mitano ya kukalia kiti cha urais?
Kwa mtazamo wa wachambuzi wa siasa, lengo la Marekani ni kuitumia Mali katika kukabiliana na wapinzani wao wakubwa, Urusi.
Ikumbukwe, kwa miaka mingi, Mali ilikuwa chini ya Ufaransa. Taifa hilo ndilo lililokuwa likituma wanajeshi wake kuingia Mali na kukabiliana na vikundi vya kigaidi.
Ilipofika mwaka 2022, Serikali ya kijeshi iliwaondosha wanajeshi wa Ufaransa, hatua hiyo ikipongezwa kwa kutajwa kuwa ni ushindi dhidi ya wakoloni. Haikuwa hivyo. Urusi ikaingia kuchukua nafasi ya Ufaransa.
Hatua ya Urusi kuingia Mali iliwapa hofu Marekani. Kwamba wapinzani wao wameongeza ushawishi na kupata ‘mwanachama’ mpya barani Afrika. Ndipo ulipokuja mpango wao wa kujisogeza Mali kwa kisingizio cha kumsaidia Jenerali Goita katika mapambano yake dhidi ya magaidi.
Wakati huo huo, maumivu ni makali kwa raia wa Mali kipindi hiki cha operesheni za usalama zinazoendeshwa na wanajeshi wa Urusi nchini humo. Mauaji ya raia yamekuwa ya kiwango cha kutisha.
Pia, Urusi imekuwa ikitumia fursa hiyo kuchota rasilimali za Mali, ikielezwa kushika sekta nyeti za uchumi wake, ikiwamo ya madini.
Hivyo, kwa kuona Urusi inayofaidi rasilimali za Mali, Marekani imeamua kutia mkono. Nayo imejitosa kushirikiana na utawala wa kijeshi wa Jenerali Goita.
Kwa lugha rahisi, Mali imegeuka uwanja wa ‘Vita Baridi’ kati ya Urusi na Marekani na mbaya zaidi, hakuna taifa lolote kati ya hayo linalojali masilahi ya raia wa nchi hiyo.
Picha inayoweza kukujia ni kwamba Mali iliondosha unyonyaji wa Ufaransa na kuiita hatua hiyo kuwa ni ushindi dhidi ya ukoloni lakini sasa imejikabidhi mikononi mwa wakoloni wawili.
Mazingira hayo ya Mali hayatofautiani sana na kile kinachoendelea kwa majirani zao wa Afrika Magharibi, Burkina Faso na Niger.
Burkina Faso chini ya kiongozi wa kijeshi, Kapteni Ibrahim Traore, iliwafukuza Wafaransa waliokuwa wakilinda amani. Haikuwa kuondosha wakoloni, bali kuikaribisha Urusi.
Ni kama ilivyo kwa Niger, ambayo pia inaongozwa kijeshi. Licha ya misimo yake dhidi ya mataifa ya Magharibi, Urusi imeweza kupenya na kuwa sehemu muhimu ya mipango ya kijeshi na kiuchumi nchini humo.
Kwa pamoja, mataifa hayo matatu yalijitoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC) na kuwa upande wa Rais wa Urusi, Vladimir Putin, alipokuwa akikabiliwa na mashitaka kwa uamuzi wake wa kuivamia Ukraine.
Kitendo cha viongozi wa kijeshi wa mataifa hayo, si tu kinalinda masilahi ya Putin na Urusi kwa ujumla, bali pia ni usaliti kwa Waafrika wanaoitegemea ICC katika kutetea haki zao dhidi ya viongozi wanaotumia vibaya madaraka yao.
Published:


