Na mwandishi wetu, Gazetini
PETER Mutharika, licha ya umri wake mkubwa wa miaka 85 na wakati mwingine afya yake ikizua mijadala, amerejea katika siasa za Malawi baada ya kukalia tena kiti cha urais kwa kumng’oa madarakani Lazarus Chakwera.
Kuanguka kwa Chakwera, kwa mujibu wa wachambuzi wa siasa, kumetokana na hali ngumu ya kiuchumi katika miaka mitano ya uongozi wake.
Mutharika, msomi wa masuala ya sheria na uchumi aliyewahi kufundisha katika vyuo vikuu vingi Afrika, Ulaya na Marekani, alikuwa mshauri wa sera za nje wakati wa utawala wa kaka yake, Bingu.
Miaka miwili baada ya Bingu kufariki mwaka 2012, akiwa ameshika nafasi mbalimbali katika Baraza la Mawaziri, alichaguliwa kuwa Rais wa Malawi. Aliondoka madarakani mwaka 2025 baada ya kuzidiwa kura na Chakwera.
Je, nini kilichomwangusha Chakwera katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu na kushuhudia Mutharika akirudi kwenye kiti cha urais?
Mwandishi wa habari aliyejikita katika masuala ya biashara, Kingsley Jassi, anasema Chakwera alishindwa kukabiliana vilivyo na tatizo la umasikini kwa wananchi wa Malawi.
Kwa miaka mitano ya uongozi wa Chakwera, Jassi anasema umasikini umeongezeka kutoka asilimia 50.77 hadi asilimia 77. Sambamba na hilo, mfumuko wa bei za bidhaa umepanda kutoka asilimia 9.9 hadi asilimia 30.
Aidha, Mavuto Bamusi, ambaye ni msomi wa masuala ya Sayansi ya Siasa, anasema rushwa, hasa katika manunuzi ya dawa na sekta ya ujenzi, vilichangia kumwangusha Chakwera.
Mtazamo wa Bamusi unaungwa mkono na msomi mwingine, Francis Mkandawire, akisema: “Wananchi wanataka sera zitakazowaondoshea mzigo wa ugumu wa maisha. Uchaguzi ulihusu zaidi hali ya kiuchumi, kama utawala mpya utashindwa kufanyia kazi, basi wananchi watapaza tena sauti zao.”
Kwa upande wao, wananchi wa kipato cha chini wanaeleza matarajio yao kwa uongozi mpya wa Rais Mutharika.
Thokozani Banda, mama wa watoto watatu mjini Lilongwe, anasema: “Nataka kuona mabadiliko ya kweli. Nataka kuona gharama za maisha zikishuka. Maisha yamekuwa magumu sana.”
Mwingine ni Anne Machesi, ambaye anajishughulisha na biashara ndogondogo. Anasema: “Ahadi hazitoshi. Kufanya biashara ndogondogo imekuwa ngumu sana kutokana na kupanda kwa bei kila wiki. Tunataka mabadiliko yatakayowezesha uhakika wa upatikanaji wa chakula na bidhaa muhimu.”
Hata hivyo, mchambuzi wa siasa, ambaye pia ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Biashara na Sayansi cha Malawi (MUBAS), Chimwemwe Tsitsi, ana mtazamo tofauti kidogo.
“Haijalishi ni nani angeshinda (kiti cha urais), itachukua muda kuondosha changamoto za kiuchumi kama vile uhaba wa mafuta na fedha za kigeni, na kupanda kwa mfumuko wa bei.
Rais Mutharika ana watoto watatu katika ndoa yake na mke wake wa kwanza, Christophine, ambaye alifariki mwaka 1990. Kwa sasa, mwanasiasa huyo ni mume wa mbunge wa zamani wa Chama cha DPP, Gertrude Maseko.
Published:


