7.6 C
New York

Dira ya Maendeleo 2050 yasisitiza malezi bora ya watoto nchini

Published:

Na Patricia Kimelemeta, Gazetini

DIRA ya Maendeleo ya Mwaka 2020-2050 imeitaka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuimarisha uchumi wa kati wa kiwango cha juu sambamba na masuala ya ustawi wa jamii, ili watoto wanaozaliwa wapate malezi bora kupitia afua tano za malezi na makuzi ya mtoto.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Khamis Abdullah Said, katika mafunzo ya waandishi wa habari wa Zanzibar kuhusu Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM) kupitia Programu Jumuishi (PJT-MMMAM), yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wa Tanzania Bara, programu hiyo ilizinduliwa mwaka 2021 na inatekelezwa hadi mwaka 2027, ikilenga watoto kuanzia umri wa sifuri hadi miaka mitano. Afua zinazotekelezwa ni Afya, Lishe, Elimu, Malezi yenye mwitikio pamoja na Ulinzi na Usalama. Serikali inashirikiana na wadau mbalimbali wakiwamo sekta binafsi na vyombo vya habari ili kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya kutosha juu ya malezi, kila mmoja akitimiza wajibu wake.

Katibu Mkuu Abdullah alisema dira hiyo imeweka mwongozo wa kuhakikisha watoto wanalelewa kupitia afua zote tano ili wakue katika utimilifu wao. Hatua hiyo itasaidia kupunguza changamoto kama vile utapiamlo, uzito pungufu na ukatili. Aidha, alisisitiza jukumu la wazazi na jamii kushiriki kikamilifu katika malezi ya watoto.

“Dira imeitaka serikali kuimarisha huduma za jamii kwa lengo la kuhakikisha watoto wanakua katika utimilifu wao. Jamii nayo inapaswa kushiriki moja kwa moja katika malezi ya watoto ili tuweze kupata viongozi bora wa baadaye, kwani jukumu la malezi ya mtoto si la serikali pekee, bali ni la kila mmoja wetu,” alisema Abdullah.

Aliongeza kuwa kwa sasa, asilimia 53 ya watoto wenye umri wa miaka 2-5 hawajafikia hali ya utimilifu, huku asilimia 47 pekee ndio waliofikia hatua hiyo. “Juhudi zaidi zinahitajika kuhakikisha watoto wanakua katika mazingira bora na salama, wakipata huduma muhimu za ukuaji kama lishe bora, chanjo, elimu na ulinzi,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Kenneth Simbaya, alisema serikali za Zanzibar na Tanzania Bara zimekuwa na ushirikiano mkubwa na vyombo vya habari kuhakikisha PJT-MMMAM inawafikia walengwa. Hali hiyo imesaidia kuwajengea uwezo waandishi wa habari ili waelimishwe na wao kuelimisha jamii kuhusu malezi.

“UTPC kwa kushirikiana na Children in Crossfire (CIC) imeweza kutoa mafunzo ya malezi ya awali (ECD) kwa waandishi nchi nzima. Kila mkoa una kinara wa malezi anayehusika kuripoti habari za watoto kwa uhalisia pamoja na kushiriki katika shughuli za malezi zinazofanywa na mikoa na kuhudhuria vikao vya tathmini ya utekelezaji vinavyofanyika kila baada ya miezi mitatu,” alisema Simbaya.

Aidha, alisema waandishi hao wanashirikiana moja kwa moja na uongozi wa mikoa katika vikao vya tathmini na kuripoti shughuli zinazotekelezwa ili kuhakikisha masuala ya ECD yanatekelezwa kwa vitendo.

Ameongeza kuwa mkakati uliopo ni kuhakikisha waandishi wengi zaidi wanapata elimu hiyo, ili wawe chachu ya kubadilisha mtazamo wa jamii na kuifanya ishiriki kikamilifu katika malezi ya watoto.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img