Na Faraja Masinde, Gazetini
“Lakini siyo mila na desturi ziangaliwe tu, bali ziachwe kabisa kwani ni hatarishi na zinachochea maambukizi ya virusi vya ukimwi, mfano hii ya kutakasa wajane ambayo inafanyika sana mikoa ya Kanda ya Ziwa, mwanamke anatafutiwa mwanaume kwa ajili ya kumtakasa bila kujua kuwa mume wake alifariki kwa ugojwa gani, hii ni hatari kubwa sana, fikiria vipi kama mume wake alifariki kwa VVU, huyu mtakasaji atabaki salama?,” Kitula.
Kwa mujibu Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania 2015-2016 uliotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu(NBS), unaonyesha kuwa asilimia 86 ya wanawake wenye umri kati ya miaka 15-49 wamewahi kusikia kuhusu ukeketaji.

Aidha, uelewa kuhusiana na ukeketaji unaongezeka kadri kiwango cha elimu kinavyoongeka.
Utafiti huo unaonyesha kuwa uelewa umeongezeka kutoka asilimia 71 kwa wanawake wasio na elimu hadi kufikia asilimia 97 kwa wenye elimu ya sekondari au zaidi.
Hii ni sawa na kusema kwamba ili kudhibiti vitendo vya ukeketaji basi hatuna budi kuwekeza kwenye elimu.
Kama taifa, tunatakiwa kutilia mkazo suala la elimu hususan kwa watoto wa kike ili iweze kuongeza uelewa zaidi miongoni mwa jamii juu ya madhara ya ukeketaji.
Kwani kwa kufanya hivyo kama taifa tutakuwa tumedhibiti aina hii inayoendelea ndani ya jamii yetu na kutengeneza taifa bora lisilo na ukatili.
Tayari Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imetangaza kufuta ada ya kidato cha tano na cha sita kuanzia mwaka huu 2022, hii ina maana kwamba kwasasa mtoto wa Kitanzania atasoma kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha sita bure.
Hatua hii pamoja na mambo mengine itasaidia kuongeza uelewa nakupunguza vitendo vya ukeketaji jambo linalotia doa ustawi wa taifa.
Hali ilivyo
Utafiti unaendelea kuonyesha kuwa, mwanamke mmoja kati ya 10 amekeketwa aidha, aina maarufu ya ukeketaji ni ile ya kukata nyama na kuiondoa(81%).
“Vitendo vya ukeketaji wa wanawake vinatofautiana kwa mikoa, ikianzia na asilimia chini ya moja (<1%) katika mikoa mingi, mpaka kufikia asilimia 58 kwa mkoa wa Manyara.
“Kiwango cha ukeketaji kinaongezeka kulingana na umri, ambapo asilimia 19 ya wanawake wenye umri wa miaka 45-49 wamekeketwa, ikilinganishwa na asilimia 5 kwa wanawake wenye umri wa miaka 15-19,” inabainisha ripoti hiyo.
Aidha, inaendelea kuchambua kuwa kwa Tanzania, ukeketaji unafanywa kipindi chote cha utoto.
Hata hivyo, wanawake wana uwezekano mkubwa wa kuripoti kuwa wamekeketwa wakiwa na umri chini ya mwaka mmoja(35%) au katika umri wa miaka 13 au umri mkubwa (28%).
Kwamujibu wa Utafiti wa TDHS-MIS wa mwaka 2015-2016 ambao ni wa nne kuwauliza wahojiwa kuhusu ukeketaji, kiwango cha wanawake waliokeketwa kimepungua tangu mwaka 1996 ambapo asilimia 18 ya wanawake walikuwa wamekeketwa. Kiwango kimepungua zaidi miongoni mwa wanawake wenye umri wa miaka 15-29.
Ukeketaji miongoni mwa watoto wa kike
Aidha, ili kufahamu kiwango cha wanawake ambao wanaendelea kukeketwa, wanawake waliohojiwa kwenye utafiti wa 2015-16 ambao wana watoto wa kike wenye miaka chini ya 15, waliulizwa kama watoto wao wamekeketwa.
Kwa ujumla, chini ya asilimia 1 ya watoto wa kike wa umri chini ya miaka 15 wamekeketwa, hata hivyo, kwa kuwa zaidi ya robo ya wanawake wenye umri wa miaka 15-49 walikuwa wameketwa katika umri wa miaka 13 au zaidi.
Bado kuna uwezekano mkubwa kwamba watoto wa kike wenye umri huu chini ya miaka 15 wanaweza kukeketwa baadae.
Mtazamo juu ya ukeketaji
Takribani wanawake wote(95%) wanaamini kwamba ukeketaji haukubaliki kidini na pia utaratibu huu unapaswa kuachwa mara moja kwani ni kinyume cha haki za binadamu.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathimini TACAIDS, Dk. Jerome Kamwela, anabainisha kuwa kumekuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ya VVU miongoni mwa wanawake ikilinganishwa na wanaume.
“Miongoni mwa changamoto ni pamoja na baadhi ya jamii kuendelea kutekeleza vitendo vya ukatili wa kijinsia kama ukeketaji, ndoa zisizo za hiari na za utotoni,” anasema Dk. Kamwela.
Mila hatarishi
Dk. Kamwela anazitaja baadhi ya mila hizo kuwa ni pamoja na ndoa za mitala / ndoa za wake wengi, ndoa bila ya utaratibu/chomolea/ nyumba nthobu na Makwava.
“Mbali na hizo pia kuna sherehe za kijamii, ngoma za unyago/usiku, sherehe za rika (mkesha), disko vumbi, chagulaga, kutakasa wajane na mila ya kufanya watoto wakishakua kulala nje ya makazi ya wazazi,” anabainisha Dk. Kamwela.
Akitolea mfano ukeketaji Dk. Kamwela anasema kuwa baadhi ya maeneo ambayo yameonekana kuendeleza sana kasi ya mila ya ukeketaji nchini ni pamoja na mikoa ya Kanda ya Kati (Dodoma na Singida), Mikoa ya Kaskazini: Arusha na Manyara na Kanda ya Ziwa hususan mkoa wa Mara.
“Lakini katika mikoa ya Dodoma na Njombe kuna wazazi wa kiume hufanya ngono na binti zao au mzazi wa kike kufanya mapenzi na mtoto wake wa kiume (MAKWAVA). Asilimia 95 ya wanawake wanaamini kwamba ukeketaji haukubaliki katika imani za dini zao na wametaka utekelezwaji wa mila hii ukomeshwe,” anasema Dk. Kamwela.
Upande wake Mkurugenzi wa Habari na Uraghibishi kutoka TACAIDS, Jumanne Issango anasema ni muda sasa kwa wataalam,waratibu wa UKIMWI na viongozi mbalimbali katika jamii kubadili ama kurekebisha mila zilizopitwa na wakati ambazo zimekuwa kichocheo cha ongezeko la maambukizi mapya ya VVU katika jamii.
“Tanzania ni kubwa na ina mila mbalimbali ambazo huwenda kwa wakati huu zinapaswa kurekebishwa ili kuendana na mazingira halisi.
“Tuangalie suala la ufuatiliaji na tathimini,tuone takwimu zinatuambiaje ili kujua wapi tuelekeze nguvu, tuangalie mila mbalimbali zilizopo ambazo zinarudisha nyuma juhudi zetu ili zibadilishwe,hatuwezi sema zote sio nzuri ila nyingine kulingana na mazingira ya sasa huwenda zinahitaji kufanyiwa marekebisho,” anasema Dk. Issango.
Jamii ielimishwe
Graciana Mushi ni Muuguzi Mshauri kutoka Jiji la Ilala, Dar es Salaam ambaye anasema kuwa rusharoho, unyago, ukeketaji na ndoa za utotoni ni baadhi ya mila ambazo zinakwamisha mapambano dhidi ya UKIMWI nchini nakwamba jamii inapaswa kuelimishwa ili kuachana na mila hizo.
Upande wake, Lucas Kitula ambaye ni Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Idara ya Falsafa na Taaluma za Dini anasema kuwa ili kuleta mabadiliko yakiwamo ya kupinga mila hatarishi, kwanza jamii inapaswa kuhusishwa kwa kupewa elimu na kujua ubaya wa baadhi ya mila na tamaduni.
“Uhusishwaji wa jamii unalenga kuhakikisha kuwa wanajamii wanakuwa makini katika kushughulikia mila, desturi, mitazamo/mawazo hatarishi na ukiukwaji wa haki za binadamu kwenye jamii, hivyo ni muhimu jamii kuelimishwa ili kupunguza mila zinazochocha maambukizi ya VVU.
“Lakini siyo mila na desturi ziangaliwe tu, bali ziachwe kabisa kwani ni hatarishi na zinachochea maambukizi ya virusi vya ukimwi, mfano hii ya kutakasa wajane ambayo inafanyika sana mikoa ya Kanda ya Ziwa, mwanamke anatafutiwa mwanaume kwa ajili ya kumtakasa bila kujua kuwa mume wake alifariki kwa ugojwa gani, hii ni hatari kubwa sana, fikiria vipi kama mume wake alifariki kwa VVU, huyu mtakasaji atabaki salama?.
“Au vipi kama huyu mtakasaji atakuwa na maambukizi ya VVU, hatuoni kama atakuwa ameambukizwa?,” anahoji Kitula.
Zinaondoa usawa
Kitula anasema kuwabaadhi ya mila na desturi hizo zimekuwa zikichochea kuondoa usawa wa kijinsia katika jamii kutokana na wanawake au wasichana kutokupewa nafani ya kufanya maamuzi yao.
“Angalia mfano kuna hizi desturi nyingine za kuozeshwa wasichana wadogo tena wanachaguliwa wanaume bila kujua afya ya mwanaume huyo, bahati mbaya zaidi mwanaume husika anakuwa na umri sawa na babu yake jambo ambalo linapaswa kupigwa vita kwa nguvu zote.
“Kwani mambo kama haya yamekuwa yakichochea vifo kwa wanawake walio wengi, hivyo hii ni hatari sana na inachochea kuwaingiza wanawake kwenye hatari ya kupata maambukizi ya VVU kwa kasi kubwa, sambamba na hilo hii inaongeza ukosefu wa usawa wa kijinsia katika jamii kwani mtoto wa kike anapoambiwa ataolewa na huyu, au mjane anapoambiwa atatakaswa na mtu ambaye bila ridhaa yao inakuwa inamnyima haki yaike ya kuamua.
“Hivyo tunaondoa usawa wa kijinsia kwa kuwanyima haki zao za kuamua, kwani wanaume hawa ambao wamekuwa wakitakasa wajane muda mwingine au kurithi wajane wamekuwa wakiingia kufanya maamuzi ya familia bila hata kuwashirikisha wanawake hawa waliowarithi,” anasema Kitula.
Mkakati wa Serikali
Oktoba 6, mwaka jana Serikali kupitia kwa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, ambaye kwasasa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ilisisitiza kufanyika kwa utafiti kuhusu mila mbalimbali zilizopo nchini lengo likiwa ni kuondoa zilizo hatarishi kwa jamii ambazo zimekuwa ni chanzo cha maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi.
Waziri Mhagama alibainisha hayo wakati wakujadili changamoto za ukatili wa kijinsia, usawa wa kijinsia, mila potofu na unyanyasaji wa kijinsia katika mwitikio wa mapambano ya VVU na Ukimwi nchini.
Kwa mujibu wa Waziri Mhagama kufanya hivyo kutasaidia kuendelezwa na kutangazwa kwa mila nzuri ikiwa ni pamoja na kutoa elimu katika jamii.
“Kutokana na changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza sababu ya mila, niwakati sasa wakufanya tafiti ili kujua ni zipi ambazo ni nzuri ili ziweze kuendelezwa na elimu ya kutosha kwa jamii itolewe na zile ambazo ni hatarishi ziachwe.
“Lakini pamoja na hayo tuangalie ni kwa namna gani utafiti huo utakuja na mwenendo mzima wa mila nchini kwasasa. Aidha, kuwepo kwa mkakati wa kushirikisha wanaume katika kupima VVU,” alisema Mhagama.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ukimwi na Dawa za Kulevya, Fatma Taoufiq anasema utafiti wa masuala ya mila unapaswa kufanyika ili kubaini mila sisizo nzuri zisiendelezwe na zilizo nzuri ziendelezwe na zitangazwe na kuzidi kutoa elimu katika jamii ili kubadili fikra ili kuondoa mila hatarishi.


