5.7 C
New York

Kenya yaongoza nguo za mitumba Afrika

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini
UTAFITI wa Taasisi ya Teknolojia ya Massachusetts (MIT) umebaini kuwa Kenya kwa sasa ndilo taifa linaloagiza kwa kiasi kikubwa zaidi nguo za mitumba barani Afrika.
Kenya imepiga hatua hiyo na kuitunika Nigeria, ambayo tafiti za awali zilikuwa zikiitaja kuwa ndiyo nchi kinara kwa uagizaji wa nguo hizo.
Kwa mwaka 2023, takwimu zinaonesha kuwa Taifa hilo la Afrika Mashariki liliingiza mitumba yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 298.
Katika soko kubwa la Gikomba, tani takribani 100,000 za nguo za mitumba hufika hapo kila mwaka na kuingiza mapato yanayotajwa kufikia Dola milioni 100.
Baada ya Kenya, kwa mujibu wa utafiti wa MIT, mataifa ya Ghana, Afrika Kusini, Uganda na Nigeria yanafuata kwa kiwango kikubwa cha uingizaji wa nguo za mitumba.
Takwimu za mwaka 2023 zinaonesha kuwa Ghana iliagiza mitumba yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 235, ikifuatiwa na Afrika Kusini (Dola milioni 227), Uganda (Dola milioni 210) na Nigeria (Dola milioni 209).
Cha kushangaza, Nigeria bado imo kwenye orodha hiyo, licha ya Serikali ya Taifa hilo la Afrika Magharibi kupiga marufuku uagizwaji wa nguo za mitumba.
Kwa upande mwingine, nguo za mitumba zimekuwa na faida kubwa si tu kwa wasafirishaji, bali ni chanzo kikubwa cha mzunguko wa fedha kwa wafanyabiashara wadogo katika mataifa hayo.
Mathalan, kwa Kenya, biashara ya kuuza nguo za mitumba si tu ni kimbilio la familia masikini katika kujisitiri, bali pia inatajwa kuwa chanzo cha kipato kwa watu zaidi ya milioni mbili.
Hata hivyo, bado utitiri wa nguo za mitumba zinazoagizwa kutoka ugharibuni unatajwa kuwa chanzo cha kudorora kwa maendeleo ya viwanda vya ndani.
Katika hilo, wapo wanaosema wingi wa mitumba unaifanya ipatikane kwa bei rahisi, hivyo nguo zinazotengezwa na viwanda vidogo vya ndani kukosa soko.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img