6.4 C
New York

Imani za kishirikina na matumizi ya viungo vya binadamu

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini
IKO hivi; kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2022 ya Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO), Taifa la Siera Leone lina idadi kubwa ya waganga wa kienyeji kuliko madaktari.
Wakati madaktari wakiwa 1,000 pekee katika Taifa hilo la Afrika ya Magharibi, waganga wa kienyeji ni zaidi ya 45,000.
Sasa, kwa siku za hivi karibuni, jamii nyingi nchini Siera Leone zimetumbukia katika mauaji yanayohusishwa moja kwa moja na imani za kishirikina.
Inaelezwa kuwa mauaji hayo yamekuwa yakienda sambamba na miili kutolewa viungo vya mwili, zikiwamo sehemu za siri, macho na mikono.
Sallay Kalokoh ni mmoja ya wahanga wa matukio hayo, ambapo anaeleza masikitiko yake baada ya kuuawa kwa mtoto wake wa umri wa miaka 11.
Kwa mujibu wa Sallay, mtoto huyo alipotea kwa wiki mbili, kabla ya mwili wake kuokotwa ndani ya kisima ukiwa umenyofolewa sehemu za siri, macho na mkono.
“Nina huzuni sana. Wamemuua mtoto wangu na hakuna hatua zozote za kisheria zilizochukuliwa,” anasema Sallay katika mahojiano yake na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).
Kwa mujibu wa uchunguzi wa BBC, mauaji hayo yamekuwa yakisababishwa na masharti ya waganga wa kienyeji kwa wateja wao, hasa wanaotaka utajiri, vyeo maeneo ya kazi au nafasi za kisiasa.
Katika uchunguzi wake, BBC ilifanikiwa kuwafikia na kufanya mahojiano na waganga wa kienyeji wawili, ambao walikiri kuwaagiza wateja wao viungo vya binadamu kama masharti ya kufanikiwa.
Walieleza pia kuwa wana mtandao mkubwa na wamekuwa wakipata wateja wengi, wakiwamo watu maarufu, kutoka ndani na nje ya Afrika ya Magharibi.
Akihojiwa na BBC, mmoja ya ‘wataalamu’ hao anayepatikana Kaskazini mwa Siera Leone, alisema:
“Nafanya kazi na wanasiasa wakubwa wa Guinea, Senegal na Nigeria. Tuna timu yetu (ya waganga) kila kinapofika kipindi cha chaguzi. Ukija hapa usiku, utakuta watu wengi sana.”
Sheku Tarawallie, Rais wa Baraza la Tiba za Asili nchini Siera Leone, licha ya kulaani vitendo hivyo, anakiri kuwapo kwa wanasiasa wanaokwenda kwa waganga wa kienyeji ili kupata nafasi za uongozi. Anasema:
“Mtu anapotaka kuwa kiongozi, anapewa sharti la kuleta viungo vya binadamu. (Waganga) wanavutumia kama sadaka. Pia, wamekuwa wakiambiwa kuwachoma watu moto na kutumia majivu au mafuta yao kupata uongozi.”
Kwa upande mwingine, vyombo vya dola vimekuwa vikitupiwa lawama kwa namna vinavyoshindwa kuja na majibu katika matukio ya watu kuuawa kwa imani za kishirikina.
Mathalan, miaka miwili iliyopita, mhadhiri wa Chuo kikuu mjini Freetown alipotea na kisha mwili wake kukutwa umezikwa katika makazi ya mmoja ya waganga wa kienyeji mjini Waterloo.
Licha ya kesi hiyo kuzua taharuki kubwa na kufikishwa Mahakama Kuu, hakuna kilichoendelea na watuhumiwa waliachiwa miezi michache tu baadaye.
Wakati huo huo, zipo taarifa kuwa baadhi ya polisi hushindwa kwenda mbali zaidi katika matukio ya aina hii, wakihofia kurogwa na wahusika (waganga wa kienyeji).

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img