LOS ANGELES, Marekani
MWAKA 2018, staa wa muziki wa Hip hop nchini Marekani, Drake, alitikisa vichwa vya habari za burudani zilipoibuka taarifa kuwa ametelekeza mtoto.
Nyota mwenzake wa Hip hop, Pusha T, ndiye aliyeibuka skendo hiyo kupitia wimbo uitwao ‘The Story of Adidon’
Katika wimbo huo, Pusha T anafichua kuwa Drake amemkataa mtoto wa kiume aliyezaa na staa wa filamu za ngono raia wa Ufaransa, Sophie Brussaux.
“Unamficha mtoto, mwache mtoto aje nyumbani. Adonis ni mtoto wako,” anasikika Pusha katika wimbo huo uliofanya vizuri kwenye vituo cha redio na Televisheni nchini Marekani.
Ikumbukwe, bibiye Sophie aliwahi kuibuka mwaka 2017 na kusema ana ujauzito wa miezi mitatu na nusu, akidai kuwa ni wa Drake.
Kupitia mahojiano yake na mtandao wa TMZ, Sophie alisema Drake amekuwa akimshawishi kututoa ujauzito huo, jambo ambalo hakukubaliana nalo.
Hata hivyo, tangu Pusha T alipofichua, Drake amekuwa karibu na mtoto huyo mwenye umri wa miaka nane. Abidon kwa sasa anafuata nyayo za baba yake katika muziki wa Hip hop.
Bow Wow
Rapa huyo mzaliwa wa Columbus, ambaye jina lake halisi ni Shad Moss, alikuwa umri wa miaka 13 tu alipoanza kupata umaarufu kwa jina la Lil’ Bow Wow.
Mwaka 2013, ndipo zilipoibuka taarifa kuwa Bow Wow ana mtoto katika mahusiano yake na mwanamitindo Joie Chavis.
Mara zote alipoulizwa kupitia mahojiano na waandishi wa habari, Bow Wow alikana kufahamu uwepo wa mtoto huyo wa kike anayefahamika kwa jina la Shai Moss.
Hata hivyo, baadaye rapa huyo alikiri kuwa Shai ni binti yake na huo ukawa mwanzo wa kumuhudumia na kuwajibika kama baba.
Justin Bieber
Akiwa bado kijana kabisa mwaka 2011, Bieber alikwaa skendo ya kukataa mtoto. Ni baada ya shabiki wake mwenye umri wa miaka 20 kusema amezaa na staa huyo.
Wakati huo, Mariah Yeater alisema alipata ujauzito baada ya kufanya mapenzi na Bieber wakiwa nyuma ya jukwaa wakati mwanamuziki huyo akiwa kwenye shoo mjini Los Angeles.
Hata hivyo, Bieber alishinda kesi hiyo baada ya kuongozana na bibiye huyo katika vipimo vya vinasaba (DNA). Ni baada ya kashikashi hiyo, akaachia wimbo uitwao ‘Maria’.
Eddie Murphy
Mchekeshaji huyo na staa wa muziki, Mel B, walianza mahusiano yao mwaka 2006. Kwa mara ya kwanza, walionekana katika mjengo wa Eddie ulioko Beverly Hills.
Baada ya Mel B kupata ujauzito, Eddie alikataa na kusema yeye si baba halali wa mtoto atakayezaliwa. “Sijui kuhusu huyo mtoto, hadi pale atakapozaliwa na kufanya vipimo vya DNA,” alisema Eddie.
Mtoto alipozaliwa na vipimo kufanyika, ilibainika kuwa Eddie ndiye baba halali. Mwigizaji huyo alilazimika kuomba radhi.
Published:


