HARARE, Zimbabwe
IFAHAMIKE kuwa Zimbabwe ni miongoni mwa mataifa 10 duniani yaliyochaguliwa kupokea kinga ya ugonjwa wa Ukimwi ya Lenacapavir. Hata hivyo, wakati wataalamu wa afya nchini humo wakifurahia na kuiita kuwa ni fursa, wapo wanaohoji gharama kubwa, upatikanaji, na hata usalama wake kwa afya za wananchi.
Lenacapavir ni kinga ya sindano ya kampuni ya Yeztugo ya Marekani, ambapo mtu atachomwa mara mbili kwa mwaka na hapo hatoweza kupata maambukizi ya ugonjwa huo.
Kinga hiyo inatarajiwa kuzifikia nchi 120 za kipato cha chini kufikia mwaka 2027, ikitazamiwa kupunguza maambukizi mapya milioni 1.3 kwa mwaka. Inaelezwa kuwa mataifa mengine, yakiwamo Kenya, Nigeria, Zambia, Uganda, Tanzania, Afrika Kusini, Eswatini na Botswana, yatafikiwa kuanzia Januari, mwaka huu.
Kabla ya kupitishwa na Shirika la Afya la Kimataifa (WHO), ilifanyiwa majaribio kwa wanawake, wasichana na kundi la wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja. Ndipo wataalamu walipobaini na kujiridhisha kuwa kinga hiyo ina ufanisi wa hadi asilimia 99 ya kuzuia maambukizi ya Ukimwi.
Zimbabwe ni miongoni mwa mataifa yenye kiwango kikubwa cha maambukizi, takwimu zikionesha kuwa watu milioni 1.3 wanaishi na virusi vya Ukimwi. Kwa Taifa hilo la Kusini mwa Afrika, mpango wa kinga ya Lenacapavir utayalenga makundi yaliyo hatarini zaidi, wakiwamo vijana wa kike, wajawazito na wanawake wanaonyonyesha.
Lakini je, wananchi wa kipato cha chini watamudu gharama za kupata kinga hiyo? Wengi wao wanasema ni matajiri pekee watakaomudu gharama ya Dola 28,000 kwa mtu mmoja kila mwaka.


