20.9 C
New York

Ni zamu ya Kane kubeba Ballon d’Or?

Published:

LONDON, Uingereza
MWANZONI mwa mwaka huu, Harry Kane alitimiza ndoto yake ya miaka mingi; kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu. Ni baada ya miaka 15 ya maisha ya soka, aliipa Bayern Munich taji la Bundesliga.
Hata hivyo, Kane aliishia kushika nafasi ya 15 katika kinyang’anyiro cha Ballon d’Or, tuzo ambayo ilitua mkononi mwa staa wa PSG, Ousmane Dembele.
Kwa upande wake, Kane mwenye umri wa miaka 32 amekuwa moto wa kuotea mbali, akifunga mabao kadiri anavyotaka, na huenda ana nafasi kubwa ya kuibeba Balloon d’Or ya mwakani.
Septemba, mwaka huu, Kane aliandika historia ya kuwa mchezaji aliyetumia mechi chache zaidi (104) kufikisha mabao 100 katika ngazi ya klabu. Kwa sasa, tayari ana mabao 104 katika mechi 108.
Msimu huu, nahodha huyo wa timu ya taifa ya England ‘Three Lions’ ameshaifungia Bayern jumla ya mabao 20 katika mechi 12 za mashindano mbalimbali.
Kwa takwimu hizo, si Lionel Messi wala Cristiano Ronaldo aliyemfikia Kane. Messi alihitaji mechi 17 kufikisha mabao 20, wakati Ronaldo alifunga idadi hiyo akiwa ameshuka dimbani mara 13.
Nyota wa zamni wa Bayern raia wa Ufaransa, Kingsley Coman, anamzungumzia Kane na namna alivyo na mchango mkubwa kwa wachezaji wenzake ndani ya uwanja.
“Harry anakufanya uwe bora unapocheza naye. Hayuko pale kwa ajili ya kufunga tu, bali kukusaidia kuwa sehemu ya mabao. Ni mmoja ya washambuliaji wa kati wazuri sana kucheza nao,” anasema Coman.
Akiwa na mabao 12 katika mechi saba pekee za Bundesliga msimu huu, Kane anaihitaji mengine 30 tu kuivunja rekodi ya Robert Lewandowski, ambaye ndiye mchezaji aliyefunga mara nyingi (mabao 41) katika msimu mmoja wa Ligi Kuu hiyo.
Je, ni wakati wa Kane kuibeba tuzo ya Balloon d’Or ya mwakani? Ili kufanikisha hilo, ni lazima aendeleze makali yake ya kufunga, awe mshindi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, pia aiongoze England kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia.
“Kwa kweli ningependa siku moja niwe mshindi (wa Ballon d’Or). Nitakuwa nimepata mafanikio binafsi, pamoja na timu kwa ujumla. Utakuwa ni msimu bora sana,” amesema Kane.
Endapo Kane ataibeba Ballon d’Or, basi atakuwa mchezaji wa kwanza wa Uingereza tangu Michael Owen alipotangazwa mshindi mwaka 2001, wakati huo akiwa mshambuliaji tegemeo wa Liverpool.
Pia, endapo Kane atafanikiwa mwakani, atakuwa Muingereza wa tano kuwa mshindi wa Ballon d’Or. Ukiacha Owen, wengine ni Stanley Matthews (1956), Bobby Charlton (1966) na Kevin Keegan (1978, 1979).
Mwisho, tangu Kane alipocheza mechi yake ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa akiwa na Bayern mwaka 2023, hakuna mchezaji barani Ulaya aliyefikia mabao yake 24 kwenye michuano hiyo.

Related articles

Recent articles