9 C
New York

Usiyoyajua kuhusu Askofu Mkuu wa kwanza mwanamke Kanisa la Anglikana

Published:

LONDON, Uingereza
KANISA la Anglikana limeandika historia baada ya kumteua Dame Sarah Mullally kuwa Askofu Mkuu wa Canterbury, akiwa ni mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo tangu Taasisi hiyo ilipoanzishwa miaka 500 iliyopita.
Dame Sara mwenye umri wa miaka 63, ni kama ameingia tena kwenye vitabu vya historia kwani alikuwa mwanamke wa kwanza pia alipoteuliwa kuwa Askofu wa London mwaka 2018.
Bi. Dame Sara, ambaye sasa anakuwa Askofu Mkuu wa 106 wa Canterbury, anafahamika kwa namna alivyohudumu kwa miaka 35 katika sekta ya afya, akijikita zaidi katika matibabu ya saratani.
Licha ya kuwa na nafasi ya juu katika sekta ya afya, ambapo alikuwa mshauri wa Serikali, aliacha kazi mwaka 2004 na kujikita moja kwa moja katika huduma ya utumishi wa Mungu.
Akianzia katika ngazi za chini, Dame Sara alipanda na hatimaye kuwa mweka-hazina wa Kanisa Kuu la Salisbury mwaka 2012. Miaka mitatu tu baadaye, aliteuliwa kuwa Askofu wa Dayosisi ya Exeter mwaka 2015.
Ilipofika mwaka 2018, ndipo alipoteuliwa kuwa Askofu wa London. Alikuwa Askofu wa tatu mkubwa wa Kanisa la Anglikana baada ya wale wa Canterbury na York.
Kwa upande mwingine, Dame Sara anafahamu ilivyo ngumu kwa jamii kumuelewa akiwa mwanamke aliyepewa nafasi ya juu zaidi katika Kanisa la Anglikana. Alizungumzia hilo alipoteuliwa kuwa Askofu wa London miaka saba iliyopita.
“Nawaheshimu sana wanaoamini kuwa mwanamke hawezi kuwa askofu. Hata hivyo, imani yangu ni kwamba Kanisa linapaswa kumpa kila mtu, bila kujali jinsia, nafasi ya kuongoza,” alisema.
Aidha, Dame Sara anafahamika kuwa ni mtu mwenye msimamo katika kile anachokiamini. Mathalan, ni mkosoaji mkubwa wa vitendo vya utoaji wa mimba. Pia, hajawahi kuficha msimamo wake wa kupinga sheria inayoruhusu mgonjwa kuuawa kwa msaada wa madaktari endapo atakubali.
Lakini, Dame Sara hakubaliani na wengi juu ya msimamo wake wa kuunga mkono mapenzi ya jinsia moja. Licha ya Serikali kuruhusu, Kanisa la Anglikana limegawanyika juu ya kukubaliana na ndoa za aina hiyo.
Akiwa Askofu, Dame Sara alikuwa Mwenyekiti wa Bodi iliyotetea utamaduni huo, ingawa sasa ana mtihani mgumu wa kutetea hoja ya ndoa za aina hiyo kufungwa kanisani.
Pia, akiwa Askofu Mkuu kwa sasa, Dame Sara ana changamoto nyingine ya kuikabili, ambayo ni kulisafisha Kanisa la Anglikana kutokana na tuhuma nyingi za unyanyasaji wa kingono zilizosababisha mtangulizi wake, Justin Welby, kutangaza kujiuzulu Novemba, mwaka jana.
Kama itakumbukwa, Welby alilazimika kung’atuka baada ya kashfa ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto wa kiume zaidi ya 120. Alisema amejiweka kando kwa nia ya ‘kuwafuta machozi’ waathirika wote wa vitendo hivyo.
Kama hiyo haitoshi, kutokana na presha kubwa kutoka kwa waumini na wakosoaji wake, Bodi inayohusika na utungaji wa sheria za Kanisa la Anglikana ilipitisha fidia ya Pauni milioni 150 kwa wahanga wa udhalilishaji wa kingono.
Haijasahaulika pia, wanaharakati wa haki za watoto (IICSA) walienda mbali zaidi na kuitaka Serikali ya Uingereza kuingilia kati matukio ya udhalilishaji wa kingono ndani ya Kanisa hilo.
Kwa sheria za sasa za Kanisa, masuala yote ya aina hiyo, kwa maana ya udhalilishaji wa kingono, hushughulikiwa ndani na si vyombo huru vya nje kama inavyotakiwa na wanaharakati.
Changamoto nyingine kubwa aliyonayo Dame Sara ni namna atakavyoshughulika na masuala ya siasa. Kwa miaka ya hivi karibuni, kumekuwapo na mpasuko miongoni mwa waumini juu ya Kanisa kujihusisha kwa kukosoa au kuunga mkono masuala ya Serikali.
Katika mpasuko huo, wapo wanaoamini Kanisa linapaswa kuingilia na kupaza sauti, kama alivyofanya Askofu Mkuu aliyepita, Welby, ambaye alipinga mpango wa Serikali wa kushughulikia wahamiaji haramu akisema operesheni yake ilikuwa ikikinzana na mafundisho ya Ukiristo.
Utafiti uliofanywa mwezi uliopita (Septemba, 2025) ulionesha kuwa wengi kati ya waumini waliohojiwa wanatamani kuona Askofu Mkuu mpya, Dame Sara, akijiweka kando au kuzungumza kwa kiasi katika masuala ya siasa za nchi ili kuepuka kuligawa Taifa.
Vilevile, ipo changamoto ya kuporomoka kwa ushawishi wa Dini ya Ukiristo. Kwa mara ya kwanza, idadi ya Wakiristo, kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2021, ni ndogo zaidi (46.2%) katika Visiwa vya England na Wales nchini Uingereza.
Takwimu hizo zinaonesha kuwa idadi ya waumini wa Dini hiyo imeshuka kwa asilimia 33.3, ukilinganisha na majibu ya Sensa ya mwaka 2011. Anguko hilo linaonekana pia katika idadi ya waumini wanaohudhuria ibada kanisani.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img