Mwandishi Wetu, Gazetini
MTAFITI maarufu duniani wa maisha ya wanyama, hususan sokwe, Dk. Jane Goodall, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 91 nchini Marekani.
Taarifa ya kifo chake imetolewa na taasisi aliyoiunda, The Jane Goodall Institute, yenye makao makuu mjini Washington D.C., ikibainisha kuwa mwanasayansi huyo alifariki kutokana na sababu za kiasili akiwa jimboni California, alipokuwa katika ziara ya kutoa mihadhara.
Dk. Goodall, aliyezaliwa Aprili 3, 1934 jijini London, Uingereza, aliingia nchini Tanganyika (sasa Tanzania) kwa mara ya kwanza Julai 14, 1960, kwa lengo la kuanzisha utafiti wa sokwe katika Hifadhi ya Taifa ya Gombe, mkoani Kigoma. Utafiti huo uliompa umaarufu mkubwa ulimwenguni, ulivunja dhana nyingi zilizokuwepo kuhusu wanyama hao, akibainisha kuwa sokwe wanatumia zana, wana hisia na mifumo ya kijamii inayofanana kwa kiasi fulani na ile ya binadamu.

Kwa zaidi ya miaka 60, Goodall alijitolea maisha yake kuchunguza uhusiano wa karibu kati ya binadamu, sokwe na mazingira, na kuibua mijadala ya kimataifa kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa misitu na wanyamapori. Hadi kufikwa na umauti, alitambulika kama mwanadamu mwenye maarifa ya kina zaidi kuhusu maisha ya sokwe.
Mbali na kuanzisha kituo cha utafiti wa sokwe Gombe ambacho hadi leo kinaendelea na tafiti za kisayansi, Goodall pia aliandika vitabu na ripoti mbalimbali zilizotafsiriwa katika lugha nyingi, huku makala zake zikipeperushwa kupitia National Geographic na kuifikisha kazi yake kwa mamilioni ya watu duniani.
Kwa mchango wake mkubwa, alitunukiwa tuzo na heshima nyingi ikiwemo National Geographic Society’s Hubbard Medal, Kyoto Prize ya Japan, na UNESCO Gold Medal. Mwaka 2002, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, alimteua kuwa Mjumbe wa Amani wa Umoja wa Mataifa.
Mbali na taaluma, Goodall alitumia umaarufu wake kuanzisha harakati za kimataifa kupitia mradi wa vijana wa Roots & Shoots, unaohamasisha vizazi vipya kushiriki katika uhifadhi na ulinzi wa mazingira.
Kifo chake kimeacha pengo kubwa katika taaluma ya sayansi ya wanyamapori na uhifadhi, huku Tanzania ikibaki kuwa sehemu muhimu ya historia yake kutokana na mchango wa kipekee alioufanya kupitia tafiti za sokwe Gombe – ambazo zimeendelea kuwa rejea ya kipekee kwa wanasayansi wa kizazi cha sasa na kijacho.


