NEW YORK, Marekani
LIONEL Messi ameendelea kuthibitisha upekee wake katika ulimwengu wa mchezo wa kandanda, licha ya umri mkubwa wa miaka 38 alionao.
Katika mechi yao dhidi ya Austria, Messi alifunga mabao yote na kuiwezesha Argentina kushinda 2-0.
Ni mchezo wa usiku wa jana Juni 22, 2026 wa Kundi H na matokeo hayo yameipeleka Argentina hatua ya 32 Bora ya fainali za Kombe la Dunia.
Kwa mabao yake hayo, Messi amevunja rekodi nne kwa mpigo, kwa mujibu wa Guiness World Records.
Kwanza, amekuwa ndiye mchezaji mwenye mabao mengi (18) katika historia ya fainali za Kombe la Dunia tangu zianzishwe mwaka 1930.
Pili, Messi amekuwa mchezaji aliyecheza mechi nyingi (28) katika historia ya mashindano hayo ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Tatu, nyota huyo wa Inter Miami ya Ligi Kuu nchini Marekani (MLS) amekuwa ndiye mchezaji aliyeshinda mechi nyingi (18) tangu michuano hiyo ianzishwe.
Nne, Messi ameweza kuandika historia ya kuwa mchezaji aliyecheza dakika nyingi (2,489) za Kombe la Dunia.
Hiyo ilikuwa ni mechi ya pili kwa Argentina msimu huu wa michuano hiyo na sasa imevuka hatua ya makundi ikiwa na mechi moja mkononi (dhidi ya Jordan).


