Na mwandishi wetu, Gazetini
JINA la Anutin Charnivirakul si geni nchini Thailand. Ni mwanasiasa mkongwe na hivi karibuni aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu baada ya kura zilizopigwa na Bunge la nchi hiyo.
Charnivirakul mwenye umri wa miaka 58, anachukua nafasi ya Paetongtarn Shinawatra, ambaye inafahamika kuwa ‘alitumbuliwa’ kwa amri ya Mahakama mwezi uliopita.
Kabla ya uteuzi wa sasa, Charnivirakul alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, pia akiwahi kushika nyadhifa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ile ya Waziri wa Afya kuanzia mwaka 2019 hadi 2023.
Akiwa na nafasi hiyo, atakumbukwa kwa uamuzi wake wa kuhalalisha matumizi ya dawa za kulevya aina ya bangi katika sekta ya afya. Thailand ikawa taifa la kwanza barani Asia kufanya hivyo.
Ni kutokana na hatua yake hiyo ya mwaka 2022, vyombo vya habari vya Thailand na hata vya nje ya Taifa hilo vilimpachika jina la ‘Mfalme wa bangi’.
Je, ni changamoto zipi zilizo mbele ya bilionea huyo anayemiliki moja ya kampuni kubwa za ujenzi nchini Thailand, Sino-Thai?
Katika hotuba yake muda mfupi baada ya kuchaguliwa kwa kura nyingi bungeni, Charnivirakul alianika vipaumbele vyake. Ni vipi hivyo?
Alisema atajikita katika kukabiliana na changamoto ya kupanda kwa gharama za maisha, mgogoro unaoendelea kati yao na majirani Cambodia, na biashara haramu ya dawa za kulevya.
Pia, Charnivirakul alionesha kuanza kuufanyia kazi mpasuko uliopo bungeni kati ya wanawasiasa wa upinzani na wenzao wa Chama tawala. “Niwaombe wabunge wote kuweka kando tofauti zao na kutanguliza masilahi ya wananchi,” alisema.
Vilevile, kuna changamoto ya kiuchumi. Takwimu za Benki ya Dunia (WB) zinaonesha kuwa uchumi wa Thailand uko kwenye hali mbaya, ambapo ukuaji wake kwa mwaka huu ni asilimia 1.8 pekee.
Hata hivyo, juu ya mgogoro wao na Cambodia, ni kama vile Charnivirakul ameshaanza kupiga hatua ya ushindi baada ya kile alichokisema Waziri Mkuu wa majirani zao hao, Hun Manet.
Akimpongeza baada ya uteuzi, Manet alimtaja Charnivirakul kuwa ni ‘karata ya ushindi’ katika mgogoro wa kugombea mipaka unaoendelea kati ya mataifa hayo.
Published:


