Na mwandishi wetu, Gazetini
UNAFAHAMU nini kuhusu ‘NepoKids’? Huo ni msamiati mpya na maarufu zaidi wakati huu wa maandamano makubwa ya raia wanaoipinga Serikali iliyoko madarakani.
NepoKids, kwa maana ya ‘Watoto wa Nepal’, ni kaulimbiu inayotumiwa na waandamanaji kuikimbusha Serikali juu ya watoto wa familia za kimasikini.
Kuibuka kwa neno hilo kulitokana na video mbalimbali zilizosambaa mitandaoni zilionesha watoto wa familia za viongozi wakiishi maisha ya anasa.
Video zilizopo TikTok na Instagram zinaanika maisha mazuri ya watoto wa viongozi, ikiwamo nguo za gharama kubwa, safari za nje ya nchi na magari ya kisasa.
Yote hayo yanafanyika wakati watoto wa familia za kipato cha chini wakisota kwenye ugumu wa maisha unaotokana na uhaba wa ajira, wengi wao wakilazimika kukimbilia nje ya nchi ili kujinasua kwenye mtego wa umasikini.
Aidha, waandamanaji wamekasirishwa na maisha hayo ya starehe ya watoto wa wanasiasa, wakati huu Nepal ikiwa kwenye hali mbaya ya kiuchumi, pia viongozi wakimezwa na skendo za rushwa.
Hatua mbaya zaidi kuchukuliwa na Serikali na kutajwa kuwakasirisha wananchi ni ile ya kufungia mitandao ya kijamii nchini humo kwa madai ya kukiuka matakwa ya kisheria.
Maandamano hayo ambayo wahusika wake wengi ni vijana wenye umri kati ya miaka 18 hadi 30, yamesababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu, ikiwamo kuchomwa kwa ofisi za Bunge.
Wakati huo huo, vurugu hizo za raia zilienda mbali zaidi na kuharibu nyumba za wanasiasa, ikiwamo ya Rais na Waziri wa Mambo ya Ndani, Ramesh Lekhak.
Sambasamba na hayo, pia vyombo vya dola vimeingia kwenye lawama vikitajwa kutumia nguvu kubwa iliyosababisha vifo vya watu 19 na wengine takribani 150 wakiachwa na majeraha.
Mapema wiki hii, Waziri Mkuu, Khadga Prasad Oli, alilazimika kuachia ngazi, hatua inayoibua wasiwasi mkubwa juu ya mwelekeo wa siasa za Taifa hilo la barani Asia.
Published:


