Na mwandishi wetu, Gazetini
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dk. Jim Yonazi, amesema maandalizi ya Michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) 2027 yanapaswa kuangaliwa zaidi ya mpira wa miguu, akieleza kuwa ni fursa ya kipekee ya kuitangaza Tanzania kimataifa, kukuza utalii, kuvutia uwekezaji na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Dk. Yonazi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Makatibu Wakuu ya Maandalizi ya AFCON 2027, amesema hayo Julai 1, 2026, wakati wa ziara ya kamati hiyo ya kukagua maendeleo ya maandalizi ya michuano hiyo katika viwanja na miundombinu mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Amesema mafanikio ya AFCON hayatapimwa kwa ubora wa mashindano pekee, bali pia kwa namna Tanzania itakavyotumia jukwaa hilo kujitangaza duniani na kuongeza mapato kupitia sekta mbalimbali za uchumi.
“AFCON 2027 ni zaidi ya mashindano ya soka; ni jukwaa la kuitangaza Tanzania duniani. Kila taasisi inapaswa kutekeleza wajibu wake ili kuhakikisha nchi inanufaika ipasavyo na fursa hii,” amesema Dk. Yonazi.
Kutokana na umuhimu huo, ameielekeza Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kuandaa mkakati maalumu wa kutangaza vivutio vya utalii, urithi wa utamaduni na fursa za uwekezaji kwa maelfu ya wageni watakaowasili nchini wakati wa michuano hiyo.
Katika ziara hiyo, Kamati ya Makatibu Wakuu ilikagua maendeleo ya maboresho katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Benjamin Mkapa Stadium pamoja na viwanja vya mazoezi vya Law School, Leaders Club, Gymkhana na Farasi ili kujiridhisha na utayari wa miundombinu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Boniface Tamba, amesema maandalizi yanaendelea kwa kasi, huku maboresho ya viwanja na ujenzi wa barabara zinazoingia na kutoka kwenye vituo vya michezo ukiwa katika hatua za mwisho.
Kamati hiyo itaendelea na ukaguzi wa maandalizi Zanzibar kabla ya kuhitimisha ziara yake katika viwanja vya michezo vilivyopo jijini Arusha, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha Tanzania inakuwa tayari kuandaa kwa mafanikio mashindano makubwa zaidi ya soka barani Afrika mwaka 2027.


