Na mwandishi wetu, Gazetini
SARATANI ya kongosho ni ugonjwa unatajwa kusababisha vifo zaidi ya 10,000 kila mwaka. Ni wastani wa mtu mmoja kupoteza maisha kila baada ya dakika 60.
Kufikia mwaka 2040, idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka zaidi na huenda wagonjwa wa saratani ya kongosho wakafikia 201,000.
Takwimu hizo zinaufanya kuwa ni miongoni mwa magonjwa hatari duniani, huku wavutaji wa sigara wakielezwa kuwa wako hatarini zaidi kupata ugonjwa huo.
Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Afya cha Michigani nchini Marekani umeeleza kuwa kemikali zilizopo katika sigara husababisha saratani ya kongosho.
Utafiti wao uliochapishwa katika jarida la Cancer Discovery, ulihusisha wagonjwa wa saratani wa aina mbili; wanaovuta sigara na wasiotumia kabisa.
Katika utafiti wao, wataalamu wa Taasisi hiyo ya afya walibaini kuwa kemikali za sigara huathiri namna uvimbe uliopo mwilini, hivyo kusababisha ukuaji wa saratani.
“Ilishangaza sana kuona uvimbe (kwa mtu anayevuta sigara) hukua haraka mno,” alieleza sehemu ya ripoti ya utafiti huo.
Wakati huo huo, tafiti mbalimbali juu ya saratani ya kongosho zimeeleza kuwa mgonjwa anaweza kuishi si zaidi ya mwaka mmoja na hiyo ni endapo tu dalili zitaonekana mapema na kuanza matibabu.
Mbaya zaidi, dalili za awali za saratani ya kongosho ni pamoja na kukosa hamu ya kula, kupungua uzito na kukosa choo, ambazo huenda zikapuuzwa na wakati mwingine kuhusishwa na magonjwa mengine.
Hivyo, endapo itafikia hatua ya ugonjwa huo kusambaa mwilini, basi ni mgonjwa mmoja tu kati ya 10 anayeweza kuishi mwaka mmoja.
Licha ya kwamba bado wengi wanaopata ugonjwa huo ni wenye umri zaidi ya miaka 75, kundi la vijana nalo linatajwa kuwa hatarini kwa sasa.
Mfano; ripoti ya mwaka jana ya Gazeti la Daily Mail ilieleza kuwa kumekuwapo na ongezeko la hadi asilimia 200 ya wanawake wenye umri chini ya miaka 25 wanaopata ugonjwa wa saratani ya kongosho nchini Uingereza.
Published:


