LAGOS, Nigeria
WANAMUZIKI wa Afrobeat, Wizkid na Tems, ni wasanii pekee wa Afrika walioingia kwenye ‘Top 500’ ya Apple Music kwa upande wa nyimbo zilizosikilizwa zaidi kwenye mtandao huo.
Orodha hiyo ya nyimbo 500 zilizosikilizwa zaidi kwa muda wote wa miaka 10 ya mtandao huo ilianikwa hivi karibuni.
Wizkid amepenya kwenye orodha hiyo baada ya wimbo alioshirikishwa na Drake mwaka 2016, ‘One Dance’, kushika nafasi ya sita.
Pia, wimbo wa Future uitwao ‘Wait For U’, ambao ndani yake ameshirikishwa Tems na Drake umekamata nafasi ya 42 kwenye listi hiyo.
Kwa upande mwingine, wimbo uliokamata nafasi ya kwanza ni ‘Shape of You’ wa staa wa muziki wa Uingereza, Ed Sheeran.
Aidha, nafasi ya pili imeshikwa na ‘Blinding Lights’ wa staa The Weeknd, huku ngoma kali ya Drake iitwayo ‘God’s Plan’ ikishika namba tatu.
Published:


