Na Mwandishi Wetu, Gazetini-Dodoma
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dk. Jim Yonazi, amewahimiza watumishi wa umma kujenga utamaduni wa kujifunza kwa bidii ili kuongeza ufanisi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali.
Dk. Yonazi alitoa wito huo leo Juni 1, 2025, jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Mfumo wa Usimamizi wa Utekelezaji na Tathmini ya Mpango wa Serikali (PEPMIS), yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Ngome.
Akinukuu kauli maarufu ya Benjamin Franklin isemayo “Niambie nisahau, nifundishe nitakumbuka, nishirikishe nijifunze,” Dk. Yonazi amewahimiza washiriki kujihusisha kikamilifu ili kupata maarifa ya kina yatakayoboresha utendaji kazi wao.
“Tuchukue sehemu ya tatu ya kauli hiyo kwa sababu tunachohitaji ni kujihusisha ili tuweze kujifunza zaidi na kuimarisha utendaji wetu,” alisema Dk. Yonazi.
Ameongeza kuwa mfumo wa PEPMIS ni nyenzo muhimu katika kufanikisha tathmini ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo, hivyo kila mtumishi anapaswa kulitumia ipasavyo ili kuongeza ufanisi wa utumishi wa umma.
Kwa upande wake, Mkufunzi wa Kitaifa wa mfumo huo kutoka Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Mutani Josephat Manyama, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa kujenga uwezo kwa watumishi wa umma kuhusu tathmini ya utendaji kazi.

Amebainisha kuwa mfumo wa PEPMIS utawezesha viongozi kufanya maamuzi sahihi ya kiutumishi, kwa kuwa utatoa takwimu na taarifa za kuaminika kuhusu utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya watumishi.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwajengea uwezo washiriki kutumia PEPMIS kama chombo cha kuboresha tija, uwajibikaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.


