Na Malima Lubasha, Gazetini – Serengeti
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kwa kupata hati inayoridhisha katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2023/2024, akisema hatua hiyo ni ushahidi wa juhudi kubwa za usimamizi wa fedha na rasilimali.
Akizungumza katika kikao maalum cha Baraza la Madiwani kilichofanyika Juni 14, 2025, kwa ajili ya kujadili hoja za ukaguzi, Kanali Mtambi amesema hatua hiyo inaonesha namna menejimenti, madiwani na watumishi walivyoshirikiana kwa ukaribu kuhakikisha matumizi ya fedha za umma yanasimamiwa ipasavyo.

“Halmashauri ya Serengeti kwa bahati mbaya ilipata hati yenye mashaka mwaka wa fedha 2022/2023 kutokana na mapungufu mbalimbali, yakiwemo malipo yenye mashaka kwa wazabuni wasio kwenye orodha rasmi. Lakini kwa mwaka huu wa fedha, mmepata hati inayoridhisha, hongereni sana,” amesema Kanali Mtambi.
Aidha, RC Mtambi ametoa wito kwa halmashauri hiyo kuendelea kuimarisha mifumo ya ndani na kudhibiti hoja za ukaguzi ili katika mwaka wa fedha wa 2024/2025 wapate hati safi.
Ameipongeza pia halmashauri kwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa asilimia 106. “Mpaka kufikia Mei 31, 2025, mlikuwa mmekusanya Sh bilioni 5.8 dhidi ya lengo la Sh bilioni 4.7. Hongereni kwa kazi nzuri,” alisema.
Katika hatua nyingine, Mtambi ameagiza Baraza la Madiwani kukaa na kuandaa mpango kazi wa utekelezaji wa maagizo ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, ambapo kati ya maagizo sita yaliyotolewa, ni moja tu lililotekelezwa kikamilifu, huku matano yakiwa bado katika hatua mbalimbali.
Amewataka madiwani kushirikiana na menejimenti kuibua vyanzo vipya vya mapato na kuimarisha usimamizi wa vyanzo vilivyopo ili kuongeza mapato ya ndani kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo na uendeshaji wa halmashauri.
Pia ametoa maagizo maalum kuhusu:
Mapato: Fedha zote zinazokusanywa zipelekwe benki kwa mujibu wa sheria na hatua zichukuliwe kwa wale wanaokiuka utaratibu.
Manunuzi: Ununuzi wa bidhaa, huduma na kazi uzingatie mfumo wa NeST, sheria ya manunuzi Sura 410 ya 2023, na bidhaa za afya zinunuliwe kupitia MSD. Kibali cha MSD kitumike endapo bidhaa hazipatikani humo.
Wazabuni wa ndani: Madeni yao ya muda mrefu yalipwe ili waweze kujenga mitaji na kuchangia maendeleo ya kiuchumi.
Mikopo ya 10%: Baraza lihakikishe linaendelea kutenga na kutoa mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, pamoja na kukusanya madeni ya nyuma ili kuwezesha mfuko huu kuwa endelevu.
Mtambi alihitimisha kwa kuhimiza uwajibikaji wa pamoja kati ya madiwani, menejimenti na watumishi wa halmashauri ili kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa ufanisi, tija na kuleta maendeleo kwa wananchi wa Serengeti.


