5.9 C
New York

Wizara ya Ulinzi kuanza kufufua viwanda kwa ushirikiano na sekta binafsi

Published:

Na Ramadhan Hassan, Gazetini-Dodoma

Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) imesema inaweka mkazo kwenye ushirikiano na sekta binafsi katika kufufua viwanda vya kimkakati vilivyokufa, ili kuhakikisha upatikanaji wa teknolojia na mitaji kwa ajili ya kuchochea uchumi wa Taifa.

Kauli hiyo imetolewa leo, Mei 22, 2025, jijini Dodoma na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Stergomena Tax, wakati akiwasilisha taarifa ya mafanikio ya wizara hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Amesema kuwa viwanda ni sehemu ya sera ya kitaifa ya maendeleo ya viwanda, hivyo Jeshi la Kujenga Taifa litaendelea kushirikiana na sekta binafsi kufanikisha azma hiyo ya kufufua viwanda hususan vile vyenye umuhimu wa kimkakati kwa Taifa.

“Tutachagua viwanda vya kimkakati ambavyo tunaweza kushirikiana na wadau kuviendeleza. Mwelekeo wetu sasa ni kushirikiana na sekta binafsi ili kupata teknolojia, mitaji na kuchangia uchumi wa nchi,” alisema Waziri Dk. Tax.

Aidha, Waziri huyo ametoa onyo kwa wananchi wanaovamia maeneo ya kijeshi, akisema kufanya hivyo kunaweza kuwa hatarishi kwa maisha yao kwani shughuli nyingi zinazofanyika kwenye maeneo hayo si za kawaida.

“Nitoe rai kwa Watanzania. Wengine wanajua kabisa hii ni ardhi ya Jeshi lakini wanaingia kwa nguvu. Jeshi linahitaji maeneo ya kufanya kazi. Kumbuka, kazi zinazofanyika mule si lazima uzione kwa macho yako – ukiingia unaweza kuathirika,” alionya.

Mafanikio Katika Kukabiliana na Majanga

Katika mafanikio ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, Dk. Tax amesema Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limehusika katika zaidi ya shughuli sita kubwa za uokoaji ndani na nje ya nchi, ikiwa ni sehemu ya kushirikiana na mamlaka za kiraia kukabiliana na maafa.

“Tumeimarisha uwezo wa JWTZ kushiriki shughuli za uokoaji na kukabiliana na majanga. Kwa kipindi cha miaka minne, tumeshiriki kikamilifu kwenye matukio makubwa kwa kutoa msaada wa uokoaji na misaada ya kibinadamu,” amesema Dk. Tax.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, hatua hizi zinaakisi dhamira ya serikali kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi pamoja na kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia ushirikiano wa kijeshi na kiraia.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img