NEW YORK, Marekani
MABAO mawili ya Kylian Mbappe na moja la Bradley Barcola yalitosha kuipa timu ya soka ya Ufaransa ushindi wa 3-1 dhidi ya Senegal.
Katika mchezo huo wa kwanza kwa kila timu msimu huu wa Kombe la Dunia uliochezwa kwenye Uwanja wa MetLife, Senegal walipata bao la kufutia machozi kupitia kwa Ibrahim Mbaye.
Kwa ushindi huo, Ufaransa imefuta rekodi yake mbaya ya kuangukia pua mara kadhaa katika mechi zake dhidi ya timu za Afrika.
Itakumbukwa, Ufaransa ilitandikwa bao 1-0 na Senegal katika mechi ya kwanza ya fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2002 zilizofanyika barani Asia.

Wakishiriki kwa mara ya kwanza Kombe la Dunia, ‘Simba wa Teranga’ walipata bao pekee hilo kupitia kwa Papa Bouba Diop (sasa marehemu).
Kwa nyakati tofauti, Nigeria, Afrika Kusini, Tunisia na Ivory Coast ziliwahi kuiduwaza Ufaransa, licha ya rekodi za jumla kuonesha kuwa mabingwa hao mara mbili wa Kombe la Dunia (1998 na 2018) wanaongoza kwa kuzifunga timu za Afrika.
Nigeria ilikuwa timu ya pili baada ya Senegal kupata ushindi mbele ya Ufaransa. Mechi ya kirafiki ya Juni 2, 2009 iliyochezwa Saint-Etienne.
Afrika Kusini walifuata kwa ushindi wa mabao 2-1 katika mchezo wa fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2010 uliochezwa mjini Bloemfontein.
Mwaka 2022 (Novemba 30), Tunisia nayo iliingia kwenye historia ya kuifunga Ufaransa. Ushindi wa bao 1-0.
Juni 4, 2025, katika mchezo wa kirafiki kuelekea fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu, Les Blues waliangukia tena pua mbele ya Afrika, safari hii wakitandikwa na Ivory Coast.
Hivyo, kwa kuifunga Senegal mabao 3-1, Ufaransa haikutaka kupoteza kwa mara ya sita mbele ya timu za Afrika.
Takwimu za jumla zinaonesha kuwa Ufaransa imeshinda mara 16, sare saba na kufungwa mara tano katika mechi ilizocheza dhidi ya Waafrika.


