16 C
New York

WhatsApp kuja na ‘message za view once’

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini-DAR

MTANDAO wa WhatsApp umeanza kujaribu kipengele kipya kitakachowawezesha watumiaji kutuma ujumbe wa maandishi unaoweza kusomwa mara moja tu kabla ya kujifuta ‘view once message’.

Hatua hiyo, hatua hiyo inalenga kuongeza udhibiti wa faragha katika mawasiliano ya kidijitali.

Kipengele hicho tayari kinatumika kwenye picha, video na ujumbe wa sauti, lakini sasa kimeanza kupatikana kwa baadhi ya watumiaji wanaojaribu matoleo ya majaribio (beta) ya WhatsApp kwenye simu za Android.

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na WABetaInfo hivi karibuni, kipengele hicho kinapatikana kwa baadhi ya watumiaji wa toleo la majaribio la WhatsApp lenye namba 2.26.45.6.

Namna ya kutumia kipengele hicho ni kuandika ujumbe kwenye kisanduku cha mazungumzo, kisha kubonyeza na kushikilia kitufe cha kutuma ujumbe ili kuchagua chaguo la ‘view Once’.

Ujumbe ukitumwa hautaonekana moja kwa moja kwenye mazungumzo kama ujumbe wa kawaida. Mpokeaji atalazimika kuugusa ili kuufungua na kuusoma kupitia sehemu maalumu ya programu. Baada ya kuufunga, hataweza kuufungua tena.

WhatsApp pia itaweka alama inayoonyesha kuwa ujumbe umefunguliwa, hivyo mtumaji ataweza kujua kama mpokeaji ameusoma endapo amewasha huduma ya taarifa za kusomwa kwa ujumbe (read receipts).

Mbali na kujifuta baada ya kusomwa, ujumbe huo hautaweza kunakiliwa, kutumwa kwa mtu mwingine (forward) wala kuhifadhiwa na mpokeaji kupitia programu hiyo.

WhatsApp pia imeweka vizuizi vya kupiga picha ya skrini (screenshot) au kurekodi kinachoonekana kwenye skrini wakati ujumbe huo unasomwa.

Hata hivyo, kipengele hicho hakiondoi kabisa uwezekano wa taarifa kusambazwa, kwani mpokeaji anaweza kutumia simu nyingine au kamera kurekodi ujumbe unaoonekana kwenye skrini. Kwa sasa, ujumbe wa aina hiyo pia hauwezi kupangiwa muda maalumu wa kutumwa.

Ingawa kipengele hicho bado kiko katika hatua ya majaribio kwa watumiaji wachache wa Android, bado haijafahamika lini kitapatikana rasmi kwa watumiaji wote.

Kipengele hicho kinaweza kuwa na manufaa kwa watu wanaotuma taarifa binafsi au nyeti ambazo hawataki zibaki kwenye historia ya mazungumzo kwa muda mrefu.

Hata hivyo, watumiaji wanapaswa kuendelea kuwa makini kwa kuwa teknolojia ya kujifuta kwa ujumbe haiwezi kuhakikisha kuwa taarifa hizo haziwezi kurekodiwa kwa njia nyingine.

Related articles

Recent articles