Na mwandishi wetu, Gazetini-DAR
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesisitiza kuwa ujenzi na uanzishwaji wa nyumba za ibada unapaswa kuzingatia mipango ya matumizi ya ardhi na taratibu za upangaji wa miji ili kuepusha migogoro na usumbufu kwa wakazi wanaozunguka maeneo hayo.
Chalamila amesema jiji la Dar es Salaam linakabiliwa na changamoto za upangaji na matumizi ya ardhi kutokana na kasi ya ukuaji wa makazi na shughuli za kiuchumi, hivyo ni muhimu kila shughuli ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa nyumba za ibada, kutekelezwa kwa kuzingatia mipango iliyowekwa.
Amesema nyumba za ibada zinapaswa kuwa maeneo ya kufanyika shughuli za kiroho bila kuwa chanzo cha kero kwa wananchi wengine, hususan kupitia kelele zinazoweza kuvuruga utulivu wa maeneo ya makazi au shughuli zisizozingatia mazingira yanayozunguka.
Aidha, amesisitiza kuwa viongozi wa dini wanapaswa kupitia mchakato unaofaa na kupata malezi yanayostahili kabla ya kukabidhiwa dhamana ya kuongoza waumini, ili kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili na wajibu wao katika jamii.
Ameeleza kuwa katika nafasi yake ya uongozi wa Serikali, anahudumia wananchi wa dini zote bila ubaguzi, hivyo ni muhimu kuheshimu imani za kila mmoja na kulinda haki ya kila mtu kuabudu.
Hata hivyo, amesema uhuru wa kuabudu unapaswa kwenda sambamba na kuheshimu haki za wengine, utulivu wa jamii na taratibu zinazotawala matumizi ya ardhi na maendeleo ya miji.


