16 C
New York

Serikali yafunguka kilichotokea Mv Mwanza

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini-Mwanza

SERIKALI imepanga kuunda timu maalumu ya wataalamu kuchunguza chanzo cha meli ya MV New Mwanza kugonga mwamba wa Bismarck Rock katika Ziwa Victoria, jijini Mwanza, wakati wa majaribio ya kiufundi.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, CP Salum Hamduni, amesema tukio hilo limetokea majira ya saa 4:00 asubuhi, huku akihakikisha kuwa meli hiyo iko salama na hakuna madhara makubwa yaliyoripotiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya tukio hilo, Hamduni amesema meli hiyo ilikuwa imeegeshwa kwa muda mrefu na Shirika la Meli Tanzania (TASHICO) lilikuwa katika hatua za mwisho za maandalizi ya kurejesha safari zake za kawaida.

“Meli iko salama. Majaribio yaliyokuwa yakifanyika leo ni sehemu ya utaratibu wa kawaida wa kiutendaji unaosimamiwa na wataalamu wetu wa TASHICO na si mara ya kwanza kwa zoezi hili kufanyika,” amesema.

Amesema pamoja na tukio hilo, Serikali imeamua kuunda timu ya uchunguzi ili kubaini chanzo chake na kujiridhisha kuhusu usalama wa chombo hicho kabla ya kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Kwa mujibu wa Hamduni, timu hiyo itahusisha wataalamu kutoka TASHICO, wizara husika, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na mamlaka za udhibiti wa usafiri wa majini.

Amesema uchunguzi utalenga kubaini iwapo tukio hilo lilitokana na hitilafu ya kiufundi au uzembe wa kibinadamu, ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.

Mwamba wa Bismarck Rock ni eneo lenye miamba mikubwa inayojitokeza juu ya maji ya Ziwa Victoria, karibu na mwambao wa jiji la Mwanza, hivyo vyombo vya majini vinavyopita eneo hilo vinahitaji kuchukua tahadhari kubwa.

Hatua ya kufanya uchunguzi inakuja wakati TASHICO ikiwa katika maandalizi ya kurejesha huduma za meli hiyo baada ya kukaa muda mrefu bila kufanya safari za kawaida.

Related articles

Recent articles