16 C
New York

Norway yakoshwa na kasi ya umeme vijijini

Published:

Na mwandishi zetu, Gazetini-DAR

SERIKALI ya Norway imepongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vitongojini na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia mkoani Lindi, inayosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), huku mradi wa umeme ukifikia asilimia 93 ya utekelezaji.

Pongezi hizo zimetolewa Novemba 18, 2026, jijini Dar es Salaam na Naibu Mkuu wa Ushirikiano wa Ubalozi wa Norway nchini, Camilla Dannevig, wakati akipokea taarifa ya maendeleo ya miradi hiyo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy.

Dannevig amesema ameridhishwa na hatua zilizofikiwa katika kupanua upatikanaji wa umeme kwenye vitongoji na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, akipongeza REA kwa usimamizi na kasi ya utekelezaji.

Kwa upande wake, Saidy ameishukuru Serikali ya Norway kwa ufadhili na ushirikiano, akisema uwekezaji huo ni kichocheo cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa vijijini.

Amesema REA itaendelea kuongeza kasi ya kuwaunganishia wananchi umeme na kuhamasisha matumizi yake katika uzalishaji mali, biashara na shughuli za nyumbani.

Ameeleza kuwa kupitia programu za matumizi yenye tija ya umeme na nishati safi ya kupikia, REA imefikia kaya 19,700 kupitia kampeni ya nyumba kwa nyumba, zilizohamasishwa kutumia umeme katika shughuli za kiuchumi na kijamii.

Msimamizi wa Miradi wa REA, Mhandisi Deogratius Nagu, amesema mradi wa usambazaji umeme umefikia asilimia 93, huku wa uhamasishaji matumizi ya nishati safi ya kupikia ukifikia asilimia 95.

Mradi wa umeme unatekelezwa na M/s Derm Group (T) Ltd, wakati kampeni ya nishati safi ya kupikia na matumizi ya umeme katika uzalishaji mali inatekelezwa na M/s Dar Merchant Group.

Miradi hiyo inalenga kuongeza upatikanaji wa nishati, kuchochea shughuli za kiuchumi, kulinda mazingira na kuboresha afya za wananchi.

Related articles

Recent articles