Na mwandshi wetu, Gazetini
WAKILI Dickson Matata amedai kuwa mwanaharakati mtanzania Malisa GJ amekamatwa baada ya kuwasili katika mpaka wa Namanga akitokea Kenya, huku hadi sasa kukiwa hakuna taarifa rasmi kuhusu alipo wala sababu za kukamatwa kwake.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Matata, Jumatatu, Agosti 31, 2026, Malisa alikuwa akirejea nchini Tanzania kutoka Marekani ambako alikuwa amekaa kwa zaidi ya miezi tisa, baada ya kuchaguliwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kushiriki mafunzo ya uongozi.
Matata amesema Malisa alifika Nairobi, Kenya, asubuhi ya leo akiwa njiani kurejea Tanzania, lakini alishindwa kuendelea na safari ya ndege kutokana na mgomo wa wafanyakazi uliokuwa ukiendelea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta. Kutokana na hali hiyo, aliamua kutumia usafiri binafsi hadi Namanga ili kuingia Tanzania kupitia Arusha.
Amesema Malisa aliwasili Namanga majira ya saa 9:00 mchana na kwenda katika ofisi za Uhamiaji kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kuingia nchini. Hata hivyo, maafisa hao walichukua hati yake ya kusafiria na kumweleza kuwa haikusomeka kwenye mfumo, hivyo walihitaji kusubiri mkuu wa kituo hicho ambaye angeweza kushughulikia changamoto hiyo.
Kwa mujibu wa wakili huyo, Malisa aliendelea kusubiri katika ofisi hizo hadi majira ya saa 1:00 jioni, ambapo alichukuliwa na gari jeupe aina ya Double Cabin ambalo, kwa mujibu wa Matata, halikuwa gari la Polisi na kupelekwa katika Kituo cha Polisi Longido. Amesema gari hilo halikukaa muda mrefu kituoni hapo na baadaye liliondoka kuelekea upande wa Arusha.
“Mpaka natoa taarifa hii hakuna taarifa kamili za aliko Malisa GJ na nini ni sababu ya kukamatwa kwake,” amesema Matata, akiongeza kuwa simu za Malisa zimezimwa tangu alipokuwa akiondolewa Namanga.
Wakili huyo ametoa wito kwa Jeshi la Polisi na Uhamiaji kutoa taarifa kwa umma kuhusu alipo Malisa GJ na sababu za kukamatwa kwake, au kuhakikisha anaachiwa huru iwapo hakuna sababu ya kisheria ya kuendelea kumshikilia.
Pia ameitaka mamlaka kuhakikisha Malisa anapatiwa haki zake za kisheria, ikiwemo kupata fursa ya kuonana na mawakili wake pamoja na kuwasiliana na watu wengine.


