22.5 C
New York

Gari la watalii latumbukia mtoni Serengeti, wageni watoka salama

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

GARI la watalii limetumbukia mtoni katika eneo la Kogatende, Kivuko cha Nyumbu Namba Moja, ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti, huku dereva na watalii wanne raia wa Uswisi waliokuwa ndani ya gari hilo wakinusurika katika ajali hiyo.

Kwa mujibu wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), ajali hiyo ilitokea jana majira ya saa 8:00 mchana katika eneo hilo ambalo ni miongoni mwa maeneo yanayotumiwa na magari ya watalii kuvuka wakati wa shughuli za utalii ndani ya Serengeti.

Gari lililopata ajali, lenye namba za usajili T 377 BJE, linamilikiwa na kampuni ya utalii ya Nature Responsible Safari Company Limited na lilikuwa likiendeshwa na Ramadhani Miraji Mbaga, raia wa Tanzania.

TANAPA imesema dereva pamoja na wageni wote wanne walifanikiwa kutoka salama baada ya gari hilo kutumbukia mtoni.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumatatu, Agosti 31, 2026, na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi katika Kitengo cha Mawasiliano TANAPA, Catherine Mbena, imeeleza kuwa hatua za awali za kinidhamu zimechukuliwa huku uchunguzi ukiendelea kubaini mazingira ya tukio hilo.

“Hatua za awali za kinidhamu zimechukuliwa na uchunguzi wa tukio hilo unaendelea,” amesema Mbena.

Ajali hiyo imeifanya TANAPA kusisitiza umuhimu wa madereva, kampuni za utalii na wageni kuzingatia sheria na taratibu zinazotumika katika maeneo ya hifadhi, hususan wakati wa kutumia vivuko.

Kwa mujibu wa Mbena, kufuata maelekezo ya wasimamizi wa vivuko ni sehemu muhimu ya kuhakikisha usalama wa watalii na mali zao, sambamba na kupunguza usumbufu kwa wanyamapori.

TANAPA imewataka madereva na kampuni za utalii kuchukua tahadhari zote muhimu wakati wa kutumia vivuko na kufuata maelekezo yanayotolewa na wasimamizi wa maeneo hayo.

“Uzembe au ukiukwaji wa taratibu unaweza kusababisha madhara makubwa yanayoweza kuepukika kwa kufuata taratibu za Hifadhi,” amesema Mbena.

TANAPA pia imeeleza kuwa uzingatiaji wa taratibu hizo ni muhimu katika kulinda maisha ya wageni, mali pamoja na mazingira ya hifadhi na wanyamapori.

Hata hivyo, hadi uchunguzi utakapokamilika, TANAPA haijaeleza chanzo cha ajali hiyo wala iwapo kulikuwa na madhara yoyote kwa mazingira au wanyamapori katika eneo hilo.

Serengeti ni miongoni mwa maeneo muhimu zaidi ya uhifadhi na utalii nchini Tanzania, hivyo usalama wa shughuli za utalii unahitaji kuzingatia kwa pamoja usalama wa binadamu, ulinzi wa mali na uhifadhi wa mfumo wa ikolojia.

TANAPA imeendelea kuwataka wadau wote wa utalii kushirikiana na mamlaka za hifadhi kuhakikisha shughuli za utalii zinafanyika kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uhifadhi.

Related articles

Recent articles