Na mwandishi wetu, Gazetini
PAUL Biya wa Cameroon ana umri wa miaka 93. Amekuwa Ikulu tangu mwaka 1982 na sasa anatumikia muhula wake wa nane aliouanza mwaka 2025. Atamaliza Novemba 6, 2032, miezi michache kabla ya kusherehekea ‘birthday’ yake ya 100.
Kwa miezi miwili sasa, Biya amekuwa akiongoza nchi akiwa Geneva, Uswis, ambako vyanzo mbalimbali vinadai kuwa anapatiwa matibabu.
Ukiacha Biya, Yoweri Museveni, licha ya umri wake wa miaka 81, ameendelea kuiongoza Uganda tangu alipoingia madarakani mwaka 1986. Museveni anabebwa zaidi na mizizi aliyosimika kwa muda mrefu kupitia Chama chake cha National Resistance Movement (NRM).
Kwa sasa, zipo taarifa kuwa anamuandaa mtoto wake wa kiume, Muhoozi Kainerugaba, kuwa mrithi wake katika nafasi ya urais. Muhoozi ndiye Mkuu wa majeshi wa Uganda.
Wakosoaji wamekuwa wakimtaja Muhoozi kuvuka mpaka na kutoa maagizo yaliyo nje ya majukumu. Mathalan, mwanzoni mwa Julai, 2026, aliagiza kufungwa kwa baadhi ya vyombo vya habari.
Wakati huo huo, Zimbabwe inaye Emmerson Mnangagwa. Akiwa na umri wa miaka 83 kwa sasa, Rais huyo haoneshi nia ya kuondoka madarakani. Juni, 2026, Bunge lilifanya mabadiliko ya kuongeza muda wa kukaa madarakani kwa rais na mbunge, kutoka miaka mitano hadi saba.
Aidha, mabadiliko mengine yaliyopigiwa kelele na wanaharakati na wanasiasa wa upinzani ni yale ya kutaka rais achaguliwe na bunge, badala ya wananchi kama ilivyo kawaida.
Ifahamike kuwa Mnangagwa anaamini kuchaguliwa kwa njia hiyo kutamsaidia kubaki Ikulu kwani asilimia kubwa ya walioko bungeni ni wanachama wa Chama chake cha ZANU-PF.


