22.5 C
New York

BoT yawataka wasanii kuwa mabalozi wa elimu ya fedha

Published:

Na Esther Mnyika, Gazetini

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imewataka wasanii, waandaaji wa burudani, watayarishaji wa maudhui na wadau wengine wenye ushawishi kwa jamii kutumia majukwaa yao kuwa mabalozi wa elimu ya fedha, ikiwemo kuhamasisha utunzaji sahihi wa noti na sarafu pamoja na matumizi salama ya huduma za kifedha.

Wito huo umetolewa leo, Jumatatu, Agosti 31, 2026, jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Tafiti na Uchumi wa BoT, Dk. Suleiman Misango, wakati wa semina iliyowakutanisha waigizaji na wasanii kwa ajili ya kuwajengea uelewa kuhusu utunzaji wa fedha na masuala ya huduma za kifedha, ikiwemo athari za watu kukusanya amana za wananchi au kutoa mikopo bila kuwa na leseni ya BoT.

Dk. Misango amesema BoT imeamua kuwashirikisha wasanii na watayarishaji wa maudhui kwa kutambua ushawishi wao katika jamii, hususan kupitia muziki, filamu, mitandao ya kijamii na majukwaa mengine wanayotumia kuwafikia watu wengi.

“Tumekuwa tukifanya kazi hii kwenye maonesho na matukio mbalimbali, lakini tumeona wadau hawa wanaweza kutusaidia kufikisha elimu kwa jamii kwa njia bora zaidi,” amesema Dk. Misango.

Amesema utunzaji sahihi wa noti na sarafu ni muhimu kwa uchumi kwa kuwa unapunguza kasi ya kuchakaa na kuharibika kwa fedha, hivyo kusaidia kupunguza gharama za Benki Kuu katika kuchapisha na kusambaza fedha mpya.

Aidha, Dk. Misango amewataka wananchi kubadili utamaduni wa kutumia fedha nyingi taslimu katika sherehe na matukio mbalimbali, akishauri kuwa kwa zawadi kubwa za fedha, wahusika wanaweza kuhamisha fedha hizo moja kwa moja kwenye akaunti ya anayepokea zawadi badala ya kubeba kiasi kikubwa cha fedha taslimu.

Amesisitiza pia kuwa noti na sarafu za Tanzania ni sehemu ya alama za utaifa na mamlaka ya nchi, hivyo zinapaswa kuheshimiwa na kutunzwa kama ilivyo kwa alama nyingine za taifa.

Hakikisha taasisi ya mikopo ina leseni

Kwa upande wake, Afisa wa BoT kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Joseph Lubava, amewataka wananchi wanaohitaji huduma za kifedha kuhakikisha wanashirikiana na taasisi zilizo na leseni na zinazotambulika kisheria.

Lubava amesema Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha imeweka madaraja mbalimbali ya watoa huduma, yakiwemo benki za huduma ndogo za fedha, SACCOS, vikundi vya huduma ndogo za fedha na watoa huduma za mikopo, huku kila kundi likiwa na taratibu zake za usajili na usimamizi.

Amewataka wananchi wanaotaka kukopa kuhakiki kwanza uhalali wa taasisi wanayokusudia kukopa kabla ya kuingia kwenye mkataba. Pia amewashauri kusoma kwa makini masharti ya mkopo, ikiwemo riba, tozo, gharama nyingine na utaratibu wa urejeshaji.

“Ukishakopa, dawa ya mkopo ni kulipa,” amesema Lubava, huku akiwataka wananchi kuhakikisha wanachukua mikopo wanayoweza kuirejesha bila kuathiri mahitaji yao muhimu ya kila siku.

Lubava pia amewataka wasanii kutumia ushawishi wao kwa kutoa elimu sahihi kwa umma badala ya kueneza taarifa zinazoweza kupotosha wananchi kuhusu huduma za kifedha. Amesema mtu mwenye ushawishi ana uwezo wa kufikisha ujumbe kwa watu wengi ndani na nje ya nchi.

Amesema wananchi wanaweza kutumia mifumo na dawati la malalamiko la BoT kupata taarifa au kuwasilisha malalamiko kuhusu huduma za kifedha, akisisitiza umuhimu wa kutoa malalamiko mapema kabla ya kuingia kwenye mikataba yenye masharti ambayo hawayaelewi.

Naye Meneja Msaidizi wa Idara ya Usimamizi wa Huduma Ndogo za Fedha BoT, Mary Ngasa, amewataka wasanii na wadau wengine walioshiriki semina hiyo kuwa mabalozi wa elimu ya fedha kwa kutumia nyimbo, video, maudhui ya mitandao ya kijamii na majukwaa yao mbalimbali.

Ngasa amesema wananchi wanapaswa kuacha kufanya shughuli za kifedha kwa mazoea na badala yake kuhakiki usajili na uhalali wa vikundi, SACCOS na taasisi za mikopo wanazotumia, ili kujikinga na hasara na migogoro inayoweza kutokana na kushirikiana na watoa huduma wasiofuata sheria.

Related articles

Recent articles