CAIRO, Misri
AFRIKA hutumia zaidi ya Dola za Marekani bilioni 100 kila mwaka kuagiza vyakula kutoka nje, huku wataalamu wakihimiza juhudi za makusudi za kupunguza utegemezi huo.
Licha ya kuwa na ardhi yenye rutuba na inayohimili mazao tofauti, changamoto kubwa inayoikumba sekta ya kilimo barani Afrika ni njia za uhifadhi. Kati ya asilimia 30 hadi 40 ya uzalishaji wa mazao ya vyakula hupotea kabla ya kumfikia mlaji wa mwisho.
Si kutokana na ukame au magonjwa, bali hupotea kwa kukosa mazingira rafiki ya uhifadhi, pia yakipoteza thamani kutokana njia za ufungashaji zisizomudu ushindani wa soka la kimataifa.
India ni moja ya nchi zilizopiga hatua kubwa katika sekta ya kilimo kupitia Mpango wake wa ‘e-Choupal’ unaounganisha vijiji 40,000 kwa kukutana na wakulima wadogo na kuwawezesha mifumo ya kijiditali ya kufanya miamala.
Kupitia ‘e-Choupal’, wakulima hao wameunganishwa katika Chama cha Kuweka na Kukopa cha (VSLA) chenye wanachama zaidi ya milioni 30 kinachofanya kazi na mataifa zaidi ya 67.
Kupitia VSLA, wakulima si tu wanaweka akiba na kukopa, pia wapatiwa elimu ya nidhamu ya pesa, masoko, pia wakiunganishwa na mazingira ya kukuza mitaji na kupata masoko ya uhakika.
Kwa upande wa Brazil, programu ya watoto kupewa chakula shuleni nayo imekuwa na faida kwa wakulima. Kwamba imewekwa kuwa ni lazima kwa asilimia 30 ya vyakula vya shule kununuliwa kutoka wakulima wa ndani.


