BAMAKO, Mali
KWA sasa, jeshi la Serikali ya Mali liko kwenye wakati mgumu kupigana na muungano wa vikundi viwili vya kigaidi,
Azawad Liberation Front (FLA) na Jama’at Nusrat al-Islam wal-Muslimin (JNIM).
FLA na JNIM viliungana Aprili 25, 2026, lengo likiwa ni kuunganisha nguvu ili kuing’oa madarakani Serikali ya kijeshi iliyoingia kwa mapinduzi.
Ni wakati huu Serikali ya Mali ikisaidiwa na vikosi vya Urusi vilivyoweka kambi nchini humo tangu nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika ilipowatimu wanajeshi wa Ufaransa.
Itakumbukwa kuwa kuungana kwa makundi hayo kulikuja baada ya kufeli kwa Mkataba wa Amani uliosainiwa mwaka 2015 huko Algeria kati ya Serikali na FLA.
Hata hivyo, FLA na JNIM yameungana yakiwa ni makundi yenye malengo tofauti kisiasa, jambo ambalo linazua maswali mengi juu ya hatima ya urafiki huo.
Kwa upande wao, FLA wameweka wazi malengo yao, kwamba wanataka uhuru wa Azawad, jina wanalotumia kumaanisha Kaskazini mwa Mali.
JNIM wao wanajinasibisha na harakati za kuikomboa Mali kwa ujumla kwa kuiondosha Serikali inayosaidiwa na vikosi vya jeshi la Urusi.
Kiongozi mwandamizi wa FLA, Kanali Mohamed Issa, anasema kujiunga kwao na JNIM hakumaanishi kuwa wameachana na malengo yao, bali wanashirikiana dhidi ya adui yao mmoja (Serikali ya Mali).
Anasema hata wapiganaji wa JNIM wanaoshirikiana nao huko Kaskazini ni vijana wanatokea maeneo hayo, hivyo wanailinda jamii yao dhidi ya jeshi la Serikali na vikosi vya Urusi.
Naye mmoja ya viongozi wa JNIM aliyetaka kutambulika kwa jina moja, Suleiman, amesema moja ya mambo yanayowaunganisha na FLA ni nia ya kuipeleka Mali katika utawala wa sheria za Dini ya Uislam (Sharia).
Kwa pamoja, makundi hayo yanajivunia namna ushirikiano huo ulivyoyarahishia kazi ya kuratibu mashambulizi dhidi ya wanajeshi wa Serikali na Urusi katika uwanja wa vita.
Vyanzo mbalimbali vya ndani na nje ya FLA na JNIM vinaeleza kuwa vikundi hivyo vimekuwa vikipata fedha kupitia michango ya wafanyabiashara, taasisi na jamii kwa ujumla.
Kwa upande mwingine, zipo pia taarifa za vikundi hivyo kuendesha operesheni za kuteka watu na kudai fedha ili kuwaachia.


