26 C
New York

Harmonize, Kajala wanaelea anga za Cardi B, Offset

Published:

Na Hassan Mwasha

MIONGONI wa strori zinazoshika nafasi kubwa mitandaoni ni hii ya staa wa Bongo Fleva, Rajab Abdul Kahali ‘Harmonize’, kuachana na bibiye wa Bongo Movie, Kajala Masanja.

Minong’ono ya wawili hao kutemana ilianzia katika tukio la hivi karibuni, ambapo Harmonize alisema hadharani kuwa Kajala hamuheshimu. Tangu hapo, strori za wawili hao kuachana zimekuwa nyingi.

Hata hivyo, kwa wafuatiliaji wa kapo hiyo yenye ushawishi mkubwa katika tasnia ya burudani, hii haitokuwa mara ya kwanza kwa Harmonize na Kajala kuachana na wala haitoshangaza kusikia wamerudiana.

Tangu walipothibitisha uhusiano wao Februari, 2017, wawili hao wameachana na kurudiana mara kadhaa, kiasi cha wakati mwingine ‘kuwaboa’ mashabiki wao na kuonekana wanatafuta ‘kiki’.

Lakini, Harmonize na Kajala si mastaa wa kwanza duniani kuwa na mahusiano ya aina hiyo; kuachana na kurudiana mara kwa mara.

CARDI B & OFFSET

Unaikumbuka kapo ya mastaa wawili wa Hip hop, bibiye Cardi B na mshikaji anayekwenda kwa jina la Offset Uhusiano wao ulianza mwaka 2016. Mwaka uliofuata, penzi lao liliota mbawa na Cardi B akaingia mitandaoni kuwataarifu mashabiki wake, akiposti ujumbe wa ‘niko singo’.

Wakati wengi wakidhani huo ndiyo mwisho wao, Cardi B na Offset waliibuka tena na kuvishana pete mwaka huo huo (2017). Miezi michache baadaye, wawili hao wakaachana, safari hii Cardi B akimshutumu Offset kwa kuchepuka na warembo wengine.

Mwaka 2018, walionekana tena pamoja na penzi likazaliwa upya. Miaka miwili baadaye, waliachana tena, kisha wakarudiana, kabla ya kutemana moja kwa moja mwaka 2024.

Licha ya kupata watoto watatu, akiwamo wa mwisho aliyezaliwa siku moja kabla ya kuachana, wameendelea kutupiana vijembe huko mitandaoni.

BIEBER & SELENA GOMEZ

Mastaa wa muziki wa Pop na R&B, Justin Bieber na Selena Gomez, nao waliwahi kuwa na mahusiano ya aina hiyo.

Walianza kuwa wapenzi mwaka 2009 lakini waliachana miaka sita tu baadaye, kisha wakarudiana miezi michache iliyofuata.

Bieber na bibiye huyo walirudiana kwa mwaka 2027 lakini safari hii walidumu miezi michache tu na kila mmoja kushika njia yake.

Kwa sasa, Selena anatoka na mshikaji anayefahamika kwa jina la Benny Blanco, wakati Bieber amemuoa Hailey na tayari wana mtoto wao mmoja.

TAYLOR SWIFT & JAKE

Kapo nyingine ya aina ya Harmonize na Kajala ni ile ya bibiye mwenye jina kubwa kwenye muziki, Taylor Swift, na jamaa aitwaye Jake Gyllenhaal.

Kwa mara ya kwanza, waliingia kwenye mahusiano Oktoba, 2010. Miezi mitatu baadaye, waliachana baada ya Jake kutokuhudhuria sherehe ya ‘birthday’ ya Taylor.

Wiki chache baadaye, wawili hao walioneka wakipata chakula cha usiku katika moja ya migahawa, kabla ya kunaswa tena wakipiga stori wakati wa hafla ya tuzo za Oscars.

Kwa mara nyingine, penzi hilo halikudumu kwa muda mrefu na sasa Jake anatoka na mwanamitindo maarufu, Jeanne Cadieu.

ZAYN & GIGI HADID

Zayn Malik ambaye ni mwanamuziki, naye aliwahi kuwa na uhusiano usiotabirika na mwanamitindo maarufu wa Marekani, Gigi Hadid.

Waliianza safari yao ya mapenzi Novemba, 2015, lakini walidumu kwa miezi kadhaa, kabla ya kuachana Julai, 2016.

Zayn na Gigi walirudiana kwa muda mfupi, kisha waliachana tena Machi, 2018. Mwezi mmoja baadaye, walionekana wakiwa kwenye ukaribu ulioashiria wamerudiana.

Hata hivyo, waliachana kwa mara nyingine mwaka 2019, kisha wakarudiana mwaka uliofuata na kupata mtoto wa kike.

Mwaka 2021, walitemana moja kwa moja baada ya Zayn kukorofishana na mama yake Hadid, Yolanda.

J-LO, BEN AFFLECK

Ukiacha hiyo, kuna kapo ya bibiye Jennifer Lopez ‘J-Lo’ na mshikaji wake, Ben Affleck. Uhusiano wao ulianza mwaka 2002 lakini ulidumu miaka miwili tu. Waliachana wakiwa kwenye mipango ya ndoa.

Mwaka 2021, J-Lo na Ben walirudiana na kuvishana pete, kisha ndoa ikafuata miezi miwili tu baadaye. Ndoa nayo ilivunjika na sasa kila mtu anafanya mambo yake.

Related articles

Recent articles