29.1 C
New York

Mashabiki Yanga, Simba wamejiandaa na VAR?

Published:

Na Hassan Mwasha

MSIMU mpya wa Ligi Kuu Bara utaanzia Agosti 14, 2026. Ni msimu wa 2026-27, ambao utakuja na sura mpya kabisa katika historia ya soka la Tanzania.

Kwa mara ya kwanza, michuano hiyo ya ndani itashuhudia matumizi ya teknolojia ya kumsaidia mwamuzi kwa marudio ya video (VAR) ikitumika. Je, maboresho hayo yanakuja kumaliza tatizo au kuongeza kero na malalamiko juu ya waamuzi?

Miaka mingi ya hivi karibuni, waamuzi wamekuwa ‘mbuzi wa kafara’ wakati na baada ya kumalizika kwa mechi; iwe Ngao ya Jamii, Kombe la Mapinduzi, Ligi Kuu au FA.

Waamuzi wamekuwa wakibebeshwa lawama kwa madai ya kuzibeba baadhi ya timu ndani ya uwanja. Msingi wa madai hayo umejengwa katika maeneo matatu; mapenzi kwa timu, rushwa, na uzembe wa kutafsiri sheria 17 za soka na kanuni zilizopo.

Mbaya zaidi, lawama nyingi kwao zimejitokeza katika mechi zinazozihusisha Yanga na Simba na mara chache kwa timu zingine za madaraja ya kati na chini.

Wakati fulani, kwa kukosa imani nao, mamlaka ziliweza hata kuagiza waamuzi kutoka nje katika mechi zenye presha kubwa, zilizozihusisha Yanga na Simba. Waamuzi wa Bongo hawaamiki!

Je, mashabiki wa Yanga na Simba, ambao mara zote huwapa presha waamuzi wakihisi timu zao hazipaswi kupoteza, wamejiandaa kisaikolojia kukubaliana na maamuzi ya VAR, hasa inapotoa maamuzi ya kuumiza?

Au kama walivyolazimisha mamlaka kutafuta marefa wa nje mara kadhaa, safari hii wataigeukia VAR na kudai inatumika ‘kuwaua’?

Wakati huo huo, inafahamike kuwa utendaji kazi wa VAR unategemea utashi wa binadamu (refa wa kati na wenzake wanaofuatilia mchezo kupitia teknolojia hiyo).

Kwamba kama bado kuna janjajanja za rushwa, mapenzi kwa timu au uzembe, bado VAR haitoweza kumaliza tatizo, na badala yake huenda ikaongeza tu.

Mfano; litakapotokea tukio la utata, VAR hailazimishi refa kwenda kulitazama tena kupitia ‘screen’. Ni uamuzi wake na wenzake wa nje. Vipi kama wamepanga kuibeba timu fulani? Shida itakuwa pale pale.

Ni kwa maana hiyo basi, uwepo wa VAR pekee hautoshi, bali pia ni lazima usafi uanzie kwa wale watakaoitumia (mwamuzi wa kati na wenzake wa nje).

Kwa upande mwingine, VAR inakuja Tanzania wakati huu teknolojia hiyo ikiwa inaacha maswali mengi juu ya ufanisi wake katika soka la nchi zilizopiga hatua kubwa.

Tulishuhudia kilichotokea katika fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu. Kabla ya hapo, tuliona malalamiko mengi msimu uliopita (2025-26) wa Ligi Kuu ya England (EPL).

Related articles

Recent articles