NAIROBI, Kenya
WAZIRI wa Usalama wa Ndani wa Kenya, Kipchumba Murkomen, ameagiza vyombo vya usalama nchini humo kufanya uchunguzi wa kina kuhusu madai ya vurugu zilizotokea wakati wa uchaguzi mdogo wa ubunge katika eneo bunge la Ol Kalou.
Agizo hilo limetolewa huku kukiwa na taarifa za matukio ya vurugu, mashambulizi dhidi ya baadhi ya waandishi wa habari, pamoja na malalamiko ya vitendo vilivyodaiwa kuhatarisha utulivu wa zoezi la uchaguzi.
Akizungumza leo Julai 16, 2026 kuhusu hali ya usalama wakati wa uchaguzi huo, Murkomen amesema serikali ilichukua hatua za kuhakikisha amani na utulivu vinadumishwa, huku akieleza kuwa Inspekta Jenerali wa Polisi aliweka idadi ya kutosha ya maafisa wa usalama kusimamia zoezi hilo.
Hata hivyo, Waziri huyo amesema madai ya kuwepo kwa watu waliotaka kuvuruga uchaguzi huo yanapaswa kuchunguzwa kwa umakini ili kubaini wahusika na sababu za matukio hayo.
“Taarifa za watu fulani kusababisha vurugu Ol Kalou lazima zichunguzwe ili kujua waliohusika na iwapo walitumwa na mtu au kundi fulani,” amesema Murkomen.
Wakati wa zoezi la upigaji kura, baadhi ya waandishi wa habari waliripotiwa kushambuliwa na kupoteza vifaa vyao vya kazi, huku kukiwa pia na taarifa za matumizi ya mabomu ya machozi katika maeneo ya uchaguzi.
Video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha baadhi ya watu waliokuwa wamevalia kofia wakiwa ndani ya gari aina ya Toyota Land Cruiser huku wengine wakionekana wakiwa na silaha, wakijaribu kuwatawanya wapiga kura na wananchi waliokuwa wakifuatilia mwenendo wa uchaguzi katika baadhi ya vituo.
Picha nyingine zilionyesha watu waliovaa barakoa wakiwa na fimbo wakiwafukuza na kuwashambulia baadhi ya wananchi, hali iliyozua wasiwasi kuhusu usalama wa wapiga kura na uadilifu wa mchakato wa uchaguzi.
Mashuhuda wa matukio hayo walidai kuwa gari la polisi aina ya Land Cruiser lililokuwa limebeba maafisa wa usalama lilipita kwa nguvu katikati ya umati wa watu waliokuwa nje ya Shule ya Ol Kalou Comprehensive, ambapo baadhi ya wapiga kura walikuwa wamebaki baada ya kumaliza kupiga kura wakisema walitaka kuhakikisha kura zao zinalindwa.
Tukio hilo limeongeza mjadala kuhusu umuhimu wa kulinda usalama wa wapiga kura, waandishi wa habari na wadau wote wa uchaguzi ili kuhakikisha michakato ya kidemokrasia inafanyika kwa uhuru, uwazi na amani.
Serikali ya Kenya sasa inatarajiwa kupitia matokeo ya uchunguzi huo na kuchukua hatua kwa wahusika endapo itabainika kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa sheria.


