31.4 C
New York

Norway yatoa Sh bilioni 8 kuchochea matumizi ya nishati safi nchini

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

Tanzania imepata nyongeza ya nguvu katika jitihada za kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi baada ya TaTEDO – Sustainable Energy Services Organization (TaTEDO-SESO) na Ubalozi wa Norway nchini Tanzania kusaini mkataba wa ruzuku wenye thamani ya hadi Krona za Norway (NOK) milioni 30, sawa na takribani Shilingi bilioni 8 za Tanzania.

Ruzuku hiyo itawezesha utekelezaji wa Programu ya Mpito wa Nishati (Energy Transition Programme) ya kipindi cha miaka mitatu, inayolenga kuongeza upatikanaji wa suluhisho za upishi safi, kuimarisha matumizi ya nishati jadidifu na kusaidia juhudi za kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi nchini.

Mpango huo unatekelezwa wakati Tanzania ikiendelea na utekelezaji wa Mission 300 Energy Compact pamoja na Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024–2034, unaolenga kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa kwa kuhamasisha matumizi ya teknolojia bora na salama za kupikia.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini, Balozi wa Norway nchini Tanzania amesema nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza maendeleo endelevu kupitia uwekezaji kwenye nishati safi.

“Ushirikiano huu unaonyesha dhamira yetu ya kuunga mkono juhudi za Tanzania katika kuhakikisha wananchi wanapata nishati safi na endelevu. Tunaamini suluhisho za nishati safi zina nafasi kubwa katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kuboresha maisha ya jamii,” amesema Balozi huyo.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa, programu hiyo inalenga kuongeza matumizi ya teknolojia za upishi safi kwa kaya na taasisi, kupanua matumizi ya nishati jadidifu katika shughuli za uzalishaji, kujenga uwezo wa wajasiriamali na jamii, pamoja na kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika soko la nishati safi.

Akizungumza kwa niaba ya TaTEDO-SESO, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Mhandisi Estomih Sawe, amesema ruzuku hiyo ni uwekezaji wa kimkakati utakaosaidia Tanzania kufikia malengo yake katika sekta ya nishati na mazingira.

“Ruzuku hii si msaada wa kifedha pekee, bali ni uwekezaji katika mustakabali wa nishati safi nchini Tanzania. Itatuwezesha kupanua huduma za kisasa za nishati, kukuza soko la upishi safi, kuimarisha ubunifu katika nishati jadidifu na kuongeza ushiriki wa sekta binafsi,” amesema Mhandisi Sawe.

Ameongeza kuwa, matumizi ya nishati safi yana mchango mkubwa katika kukabiliana na changamoto za kimazingira, ikiwemo kupunguza uharibifu wa misitu unaotokana na matumizi makubwa ya kuni na mkaa.

“Nishati safi ya kupikia ni sehemu muhimu ya suluhisho la mabadiliko ya tabianchi. Pia inasaidia kuboresha afya za wananchi kwa kupunguza uchafuzi wa hewa ndani ya nyumba na kutoa fursa za ajira za kijani, hususan kwa wanawake na vijana,”.

Mhandisi Sawe amesisitiza kuwa mafanikio ya programu hiyo yanahitaji ushirikiano mpana kati ya Serikali, washirika wa maendeleo, sekta binafsi, taasisi za fedha, watafiti na jamii kwa ujumla.

Ameongeza kuwa TaTEDO-SESO itahakikisha utekelezaji wa programu hiyo unazingatia uwazi, uwajibikaji na matumizi yenye tija ya rasilimali ili kufikia matokeo yanayotarajiwa.

Kupitia programu hiyo, Tanzania inatarajiwa kunufaika kwa kuongezeka kwa matumizi ya nishati safi, kupungua kwa utegemezi wa kuni na mkaa, kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi, kuhifadhi misitu, kuboresha afya ya jamii na kuongeza uwekezaji katika sekta ya nishati endelevu.

Hatua hiyo imeelezwa kuwa sehemu ya jitihada pana za Tanzania kuelekea uchumi wa kijani na maendeleo endelevu yanayozingatia ulinzi wa mazingira na ustawi wa wananchi.

Related articles

Recent articles