Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro
JESHI la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro limeeleza kuwa limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 188 wa makosa mbalimbali ya jinai, huku mmoja akihukumiwa kunyongwa hadi kufa na mwingine akipewa kifungo cha maisha jela kwa makosa ya mauaji.
Hatua hiyo imefikiwa kufuatia operesheni mbalimbali za kiusalama zilizofanywa na Jeshi la Polisi mkoani humo kuanzia Juni 2026 hadi sasa, kwa lengo la kukabiliana na uhalifu na kuimarisha usalama wa wananchi.
Akizungumza leo Julai 16, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, amesema kati ya watuhumiwa waliokamatwa, kesi 26 zimekamilika katika mahakama na wahusika wamepewa adhabu mbalimbali kulingana na makosa yao.
Amesema miongoni mwa hukumu zilizotolewa, mtuhumiwa mmoja aliyekuwa akikabiliwa na kosa la mauaji amehukumiwa adhabu ya kifo, huku mwingine akihukumiwa kifungo cha maisha kwa kosa hilo hilo.
“Pia kuna mtuhumiwa mmoja aliyehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kubaka, mwingine akipewa kifungo cha miaka 20 kwa kosa la kupatikana na nyara za Serikali,” amesema Kamanda Maigwa.
Ameongeza kuwa katika kesi nyingine 22, watuhumiwa wamehukumiwa vifungo vya chini ya miaka mitano pamoja na wengine kupewa adhabu ya kulipa faini.
Kwa mujibu wa Kamanda Maigwa, operesheni hizo pia zililenga kukabiliana na makosa yanayohusiana na maadili ya jamii, ambapo watuhumiwa 60 walikamatwa kwa makosa hayo.
Aidha, amesema baadhi ya watuhumiwa walikamatwa kwa makosa yanayohusiana na dawa za kulevya, ambapo watu 13 walikutwa na jumla ya kilo 13 za bangi, huku wengine 25 wakikamatwa na kilo 555 za mirungi.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro limesisitiza kuwa litaendelea kufanya operesheni za mara kwa mara ili kudhibiti uhalifu na kuhakikisha wananchi wanaishi katika mazingira salama.


