BOGOTA, Colombia
JINA la Shakira si geni kwa wapenzi wa muziki duniani. Ni mrembo mzaliwa wa Colombia, ambaye hivi karibuni alitumbuiza katika hafla ya ufunguzi wa fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu.
Shakira, kwa kushirikiana na wasanii wnegine, akiwamo staa wa Afrobeats nchini Nigeria, Burna Boy, walifanya shoo iliyotetemesha Uwanja wa Mexico City, kabla ya wenyeji Mexico kuivaa Afrika Kusini na kushinda mabao 2-0.
Nje ya kazi, Shakira mwenye umri wa miaka 49 amekuwa na mikasa ya hapa na pale inayohusu mahusiano yake na wanaume tofauti.

Miongoni mwa wanaume aliowahi kutoka nao ni mahusiano yao kuzua gumzo kwenye vyombo vya habari ni Antonio de la Rua, ambaye alikutana naye mwaka 2000.
Miaka 11 baadaye, waliachana. Desemba, 2012, mshikaji huyo alifungua kesi mahakamani akimdai Shakira kiasi cha Pauni milioni 75 (zaidi ya Sh mil. 263 za Tanzania).
De la Rua alisema alichangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya Shakira kwa kuhusika katika mikakati na mipango ya kazi za bibiye huyo.
Shakira alikanusha na kusema jamaa alikuwa mpenzi wake na si meneja wala sehemu ya timu ya kazi. Mwaka 2013, Mahakama ilitangaza De la Rua kushindwa katika kesi hiyo.
KUTEMANA NA PIQUE WA BARCELONA
Shakira na beki wa zamani wa Barcelona, Gerard Pique, walikutana kwa mara ya kwanza katika Tamasha la muziki la Rock in Rio mwaka 2010.
Hata hivyo, waliachana mwaka 2022 wakiwa wamwebahatika kupata watoto wawili; Milan na Sasha. “Nitaendelea kumuheshimu kama baba wa watoto wangu na mtu aliyenifanya kuwa mama leo hii,” alisema.
HUYU NDIYE KIBENTENI WAKE
Ni mwigizaji Lucien Laviscount. Mshikaji ana umri wa miaka 34, hivyo ameachwa miaka 15 na staa huyo wa muziki wa Pop mzaliwa wa Colombia.
Walikutana kwa mara ya kwanza wakati Shakira anarekodi video ya wimbo wake wa ‘Punteria’ na tangu hapo wakaanzisha safari ya mapenzi.
Wiki chache baadaye, Laviscount anayefahamika kwa filamu zake za ‘Waterloo Road’ na ‘Emily in Paris’ alionekana jijini New York, Marekani, akipata chakula cha jioni na bibiye huyo.
Hata hivyo, huenda kwa sasa wawili hao hawako pamoja. Akihojiwa na Gazeti la Times mwezi uliopita (Mei, 2026), Shakira alisema: “Hakuna mapenzi kwa sasa. Hayana nafasi kwenye maisha yangu kwa sasa. Nafurahia kuwa peke yangu.”


