ACCRA, Ghana
WAKATI dunia ikitambua kuwa Michael Jackson (sasa marehemu) ndiye ‘King of Pop’, ameibuka msanii mwingine mwenye mtazamo tofauti.
Ndiyo, nyota wa muziki nchini Marekani, Ama Serwah Genfi maarufu kama Amaarae, anaamini Janet Jackson ndiye ‘Mfalme wa Pop’ na siyo Michael kama inayoaminika.
Amaarae mwenye asili ya Ghana, ambaye kwa sasa anatamba na wimbo ‘Sad Girls Love Money’, ameyasema hayo alipokuwa akizungumzia albamu ya Janet ya mwaka 1997 iitwayo ‘The Velvet Rope’.
“Kila albamu yake ni kali lakini ‘The Velvet Rope’ ni hatari zaidi. Kama ningekuwa mkubwa wakati inatoka mwaka 1997, ningekuwa narudia sana kuzisikiliza …” amesema.
Aidha, amesisitiza kuwa kwa upande wake, Janet ndiye ‘King Of Pop’, yaani Mfalme wa muziki wa Pop, jina ambalo alipewa Michael wakati wa uhai wake.


