LOS ANGELES, Marekani
TAARIFA ya Serena Williams kutaka kurejea katika tenesi imeshangaza wapenzi wa tenesi duniani kutokana na umri mkubwa wa staa huyo.
Licha ya umri wake wa miaka 44, Serena ameweka wazi kuwa anataka kurudi katika mechi za ushindani kwa kushiriki michuano ya Queen’s Club itakayoanza Juni 8, 2026 mjini London.
Ikumbukwe, ni miaka minne tangu alipotangaza kustaafu mchezo wa tenesi lakini ameonekana kutokuridhishwa na mafanikio makubwa aliyowahi kuyapata katika safari ya maisha yake ya tenesi.
MATAJI YAKE
Williams ni mmoja ya mastaa wa tenesi wenye mafanikio makubwa, ikiwa ni pamoja na kutwaa mataji makubwa (Grand Slams) mara 23.
Kwamba anashika nafasi ya pili kwa mataji mengi ya mechi za mchezaji mmoja mmoja (singles) baada ya Margaret Court.
Pia, Serena ana mataji makubwa 14 kwa upande wa mechi za wachezaji wawili (double) aliyocheza ‘pacha’ na dada yake, Venus. Wawili hao walitwaa mara tatu ubingwa (medali ya dhahabu) wa Olimpiki.
KICHAPO KILICHOMSTAAFISHA TENESI
Serena alitangaza kujiweka kando ya mchezo wa tenesi baada ya kufungwa na Ajla Tomljanovic katika mchezo wa raundi ya tatu ya US Open mwaka 2022.
Kabla ya kupoteza mechi hiyo, alitoka kufika nusu fainali ya Australian Open mwaka 2021. Taji lake la mwisho kubwa ni Australian Open mwaka 2017 akiwa na umri wa miaka 35.
HUYU HAPA MPINZANI WAKE
Katika mashindano yajayo ya Queen’s Club, Serena anatarajiwa kumvaa staa wa tenesi raia wa Canada, Victoria Mboko. Nyota huyo ana umri wa miaka 19.
Kwa upande wake, Mboko ameeleza kufurahishwa na taarifa hizo. “Kama yuko tayari kurudi, nafikiri ni juu yake kutangaza,” amesema Mboko.
Kwa sasa, Serena hafanyi tena kazi na kocha Patrick Mouratoglou, ambaye alimpa mataji 10 kati ya 23 makubwa aliyonayo.
Na badala yake, Serena anatarajiwa kuwa chini ya Jarmere Jenkins na Rennae Stubbs aliyempa taji la US Open mwaka 2022.
DAKIKA 300 ZA TIZI KILA SIKU
Taarifa za kurudi kwake zimetanguliwa na zile za staa huyo kuripotiwa kupunguza uzito. Katika mahojiano yake ya mwaka 2025, alisema amepunguza kilogramu 14 ndani ya miezi nane.
Pia, alieleza namna ambavyo amekuwa akitumia saa tano (dakika 300) kila siku kufanya mazoezi ya kukimbia, kutembea, kuendesha baiskeli na kupanda ngazi.
Vilevile, kwa ubalozi wake wa Ro, huenda Serena anatumia dawa za kupunguza uzito za kampuni hiyo inayomilikiwa na mume wake, Alexis Ohanian.


