23.5 C
New York

Mrembo aliyekaribia kuvunja ndoa ya Jay Z, Beyonce

Published:

LOS ANGELES, Marekani

RAPA Jay Z na staa wa Malkia wa muziki wa R&B na Pop, Beyonce Knowles, ni moja ya ‘kapo’ za muda mrefu na zenye ushawishi mkubwa kwenye tasnia ya burudani si tu Marekani, bali duniani kwa ujumla wake.

Beyonce na Jay Z wamekuwa kwenye ndoa kwa miaka 18,  tangu Aprili 4, 2008, ambapo wamebahatika kupata watoto watatu; Blue Ivy Carter aliyezaliwa mwaka 2012 na mapacha Rumi Carter na Sir Carter (2017).

Sasa, Mei, 2014, ndoa yao ilitikiswa na video iliyonaswa na kamera za usalama (CCTV) zilizopo katika Hoteli ya kifahari ya Standard mjini New York, Marekani.

Katika video hiyo, mdogo wa staa Beyonce, Solange, aliyekuwa amelewa, alionekana akimtolea lugha chafu, pamoja na kumrushia mateke shemeji yake, Jay Z.

Ni video ya dakika tatu na ugomvi huo ulikuja baada ya Solange, Beyonce na Jay Z kukutana katika Tamasha maarufu la Met Gala.

Baadaye, Solange na Jay Z waliyamaliza, huku familia ya Beyonce ikithibitisha kwa kusema wawili hao waliombana radhi.

Tukirudi katika Tamasha la Met Gala, miongoni mwa mastaa waliokuwa wamehudhuria siku hiyo ni mrembo Rachel Roy.

Roy alifika ukumbini akiwa na gauni alilovalishwa na mbunifu wa mavazi, Oscar Lopez, ambaye hapa anasimulia chanzo cha ugomvi wa Solange na Jay Z katika mahojiano yake na Gazeti la mtandaoni la Daily Mail.

Kwa mujibu wa Lopez, tatizo lilianzia pale Solange alipomsikia Jay Z akisifia gauni la Roy. “Dada yake Beyonce (Solange) aliona haijakaa sawa (Jay Z kumsifia mwanamke mwingine,” anasema Lopez.

Ikumbukwe, tayari zilishakuwepo taarifa zinazodai kuwa Roy, ambaye ni rafiki wa zamani wa Solange, alikuwa na mahusiano ya siri na rapa Jay Z.

Ilielezwa kuwa Roy na Jay Z walikuwa wapenzi tangu bibiye huyo alipokuwa mwajiriwa wa nafasi ya Mkurugenzi wa Ubunifu kwenye kampuni yake ya mavazi ya Rocawear.

Ripoti zaidi zinaeleza kuwa wawili hao walikuwa kwenye uhusiano tangu Roy akiwa kwenye ndoa na Damon Dash, ambaye alikuwa mshirika wa Jay Z katika kampuni hiyo.

Hata hivyo, Roy, ambaye aliondoka katika kampuni ya Rocawear mwaka 2006, amekuwa akikanusha kuwa na ukaribu wa kimahaba na bosi wake huyo.

Mwaka 2016, Beyonce aliachia wimbo ‘Sorry’ na ndani yake alitupa vijembe vilivyotajwa kumlenga moja kwa moja Roy.

Lakini, Roy alikuwa na mtazamo tofauti juu ya wimbo huo akisema haukuwa kwa ajili yake. “Hakuna ushahidi kwamba wimbo ni kwa ajili yangu,” alisema.

Related articles

Recent articles