LONDON, Uingereza
WIKIENDI hii, Washika Bunduki wa London, Arsenal, na matajiri wa Paris, PSG, watavaana katika mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Vita hiyo ya usiku wa Ulaya itaamuliwa Mei 30, 206, katika nyasi za Uwanja wa Puskas mjini Budapest, Hungary, na timu hizo zinakutana zikiwa zinatoshana nguvu – zimefungana mara mbili na sare tatu katika mechi zao saba.
PSG, mabingwa watetezi, wanasaka rekodi ya kuwa timu ya kwanza baada ya Madrid kutwaa mara mbili mfululizo taji la michuano hiyo ya Shirikisho la Soka barani Ulaya (UEFA).
Benfica, Inter Milan, Ajax, Bayern Munich, Liverpool, Nottingham Forest na AC Milan ziliwahi kutetea, lakini ni wakati ule michuano hiyo ikiitwa Kombe la Washindi barani Ulaya. Siyo Ligi ya Mabingwa.
VITA YA MABINGWA
PSG na Arsenal zitakutana zikiwa zimetoka kutwaa mataji ya Ligi Kuu, Arsenal wakifanya hivyo kwa mara ya kwanza baada ya ukame wa miaka 22, PSG wakibeba Ligue 1 kwa mara ya tano mfululizo.
Arsenal wana kumbukumbu ya kupoteza mechi zote mbili walipokutana na PSG katika hatua ya nusu fainali msimu uliopita wa Ligi ya Mabingwa.
Mwamuzi aliyetoswa Kombe la Dunia
Kuelekea mchezo wa wikiendi hii utakaochezeshwa na mwamuzi wa kati raia wa Ujerumani, UEFA imeshamgaza Daniel Siebert wa Ujerumani kuwa mwamuzi wa kati.
Huu ni mwaka wake wa 11 kuchezesha Bundesliga na wa 11 kwenye michuano ya Ulaya lakini hayumo kwenye orodha ya waamuzi watakaochezesha fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu.
Wakati huo huo, mkongwe wa Bayern Munich na timu ya Taifa ya Ujerumani, Lothar Matthaus, aliwahi kumzungumzia vibaya akisema:
“Huwa hana msimamo katika maamuzi yake. Iwe ni kona au faulo, huwa hajui afanye nini. Amekuwa akisita sana katika maamuzi. Uzuri wake ni kwamba amekuwa akikubali kukosolewa.”
Msimu huu wa Ligi ya Mabingwa, Siebert amechezesha mechi moja ya PSG (0-0 dhidi ya Bilbao) na mbili za Arsenal ((1-0 dhidi ya Sporting Lisbon, 1-0 dhidi ya Atletico Madrid).
MABEKI V WASHAMBULIAJI
Mechi hii inatafsiriwa kuwa ni vita ya mabeki (Arsenal) dhidi ya washambuliaji (PSG). Kivipi? Msimu huu wa Ligi ya Mabingwa, Arsenal wameruhusu mabao sita pekee katika mechi 14.
Uimara wa safu yao ya ulinzi unatokana na viwango bora vya mabeki William Saliba, Gabriel Magalhaes na kipa wao, David Raya.
Wanakutana na PSG ambayo imefunga mabao 44 msimu huu, ikikosa bao moja tu kuivunja rekodi ya muda wote iliyowekwa na Barcelona msimu wa 1999-2000.
PSG yenye safu kali ya ushambuliaji inayoongozwa na Ousmane Dembele, Desire Doue na Khvicha Kvaratskhelia.
ARTETA V ENRIQUE
Kocha wa kwanza kuipa Arsenal taji la Ligi Kuu ya England tangu Arsene Wenger alipofanya hivyo msimu wa 2003-04.
Kwa misimu yote miwili ya hivi karibuni, Arteta ameiwezesha Arsenal kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Msimu wa tatu ni huu, ambao wako fainali.
Endapo ataifunga PSG, Arteta atakuwa kocha wa kwanza katika historia ya Arsenal kuiwezesha timu hiyo kutwaa kwa mara ya kwanza mataji makubwa mawili (Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa) ndani ya msimu mmoja.
Hata hivyo, anakutana na Luis Enrique, kocha mwenye mataji mawili ya Ligi ya Mabingwa, moja akibeba PSG na jingine akiwa na Barcelona misimu mingi iliyopita.
Hivyo, katika fainali ya wikiendi hii, Mhispania huyo anasaka rekodi ya kuingia kwenye orodha ya makocha waliowahi kutwaa zaidi ya mara mbili ubingwa wa michuano hiyo.
Makocha walio kwenye historia hiyo ni Carlo Ancelotti aliyefanya hivyo mara tano na Bob Paisley, Zinedine Zidane na Pep Guardiola, ambao kila mmoja ana makombe matatu.
VIKOSI HIVI HAPA
PSG – Safonov, Hakimi, Marquinhos, Willian Pacho, Nuno Mendes, Zaire-Emery, Vitinha, Joao Neves, Doue, Dembele, na Kvaratskhelia.
Arsenal – Raya, Mosquera, Saliba, Gabriel, Calafiori, Rice, Lewis-Skelly, Odegaard, Saka, Gyokeres na Trossard.