MOGADISHU, Somalia
MAHARAMIA wanaoteka meli nchini Somalia wameripotiwa kunufaika na mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati ukizihusisha Marekani na Israel kwa upande mmoja na na Iran kwa upande mwingine.
Meli nyingi za biashara ya mafuta zimeshindwa kupita katika Mlango-Bahari wa Hormuz kutokana na mgogoro uliopo, hivyo kulazimika kuzunguka hadi Afrika kupitia Bonde la Somalia.
Kwa meli za mafuta zinazotumia njia hiyo kukwepa machafuko ya Hormuz, ni mzunguko ulioongeza si tu muda wa safari, bali pia gharama za bima na uendeshaji.
Kwa upande mwingine, njia hiyo imeripotiwa kuongeza kasi ya matukio ya uharamia wa meli katika Pwani ya Somalia.
Taasisi ya Uendeshaji wa Biashara ya Majini ya Uingereza (UKMTO) inaeleza kuwa meli kubwa za biashara takribani tatu zilikuwa zimetekwa kufikia Mei 12, 2026.
Kwa mujibu wa ripoti ya UKMTO, meli mbili ni za mafuta na moja ni ya mizigo iliyokuwa imebeba saruji na zilitekwa kati ya Aprili 21 na Mei 2.
UKMTO inaeleza zaidi, kwamba meli moja ilitekwa Yemen na kupelekwa Somalia, ikifahamika kuwa nchi mbili hizo zinachangia mpaka wa majini.
Somalia imekuwa kwenye mtanziko wa kiusalama kutokana na kukosa Serikali Kuu, hivyo vikundi vya maharamia wa meli vimekuwa vikitawala kwa sehemu kubwa.
Kasi ya utekejaji iliongezeka maradufu baada ya kampuni zinazomiliki meli zinazotekwa kuanza kulipa fidia ili ziachiwe. Maharamia wakaona ni biashara inayowapa mabilioni ya fedha.
Mwaka 2011, matukio ya uharamia wa meli yalifikia 237, idadi kubwa zaidi kuwahi kutokea, yakigharimu uchumi wa dunia kiasi cha Dola za Marekani bilioni 7.
Wakati huo huo, vita vya Iran vinatajwa kuongeza kwa kiasi kikubwa balaa la njaa nchini Somalia. Watu milioni sita, sawa na asilimia 31 ya idadi yote ya raia, wanakabiliwa na hali mbaya ya usalama wa chakula, huku milioni 1.9 wakihitaji msaada wa dharura.
Kamati ya Majanga ya Kimataifa inaeleza kuwa bei ya mbolea imeongezeka kwa asilimia 40 hadi 65 kwa kilogram 50 ya kiroba, hivyo kuathiri shughuli za kilimo na kupanda kwa bei ya vyakula.
Mathalan, bei ya sukari imepanda kwa asilimia 13.3, mchele ni asilimia 9.6, unga ni asilimia 16, mafuta ya kupikia ni asilimia 21.4, na maziwa ya ng’ombe ni asilimia 42.8.


