DAKAR, Senegal
RAIS WA Senegal, Bassirou Diomaye Faye, amemfuta kazi Waziri Mkuu wake, Ousmane Sonko, sambamba na kulivunja Baraza la Mawaziri.
Aidha, taarifa za Waziri Mkuu kufutwa kazi zinakuja wakati Serikali ya Senegal ikitajwa kuelemewa na madeni ya nje.
Akitangaza uamuzi huo kupitia televisheni ya Taifa, msaidizi wa Rais Faye, Oumar Samba Ba, amesema: “Rais Faye amesitisha majukumu ya Ousmane Sonko, pamoja na Mawaziri na Makatibu wa Serikali.”
Wawili hao, ambao kwa nyakati tofauti waliwahi kutupwa gerezani kutokana na siasa zao za upinzani, waliingia madarakani Machi, 2024, lakini uhusiano wao umedorora katika siku za hivi karibuni.
Miezi michache iliyopita, Sonko alisema hadharani kuwa Rais Faye ameshindwa kuiongoza Senegal na amekuwa hamsaidii kukabiliana na wakosoaji wake.


