29.1 C
New York

New Bell: Gereza lenye lebo ya muziki kwa ajili ya wafungwa

Published:

YOUNDE, Cameroon

NEW Bell ni moja ya magereza makubwa na maarufu si tu Younde na miji mingine jirani, bali Cameroon kwa ujumla. Wakati fulani, Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch liliripoti kuwa New Bell lilikuwa na wafungwa 4,700, mara nne ya uwezo wake.

Kwa mujibu wa Human Right Watch, mrundikano wa wafungwa uliwahi kusababisha vifo sita vya wafungwa kutokana na ugonjwa wa kipindupindu. Pia, mwaka 2008, Shirika hilo liliripoti tukio la walinzi wa Gereza la New Bell kuwapiga risasi wafungwa 16 waliojaribu kutoroka.

Kwa sasa, kuna jambo la kuvutia katika Gereza hilo. Achana na soko, ambapo wafungwa wanapata mahitaji mbalimbali, ikiwamo mihogo ya kukaanga. Kinachoweza kushangaza zaidi, ndani ya Gereza la New Bell kuna lebo ya muziki inayoitwa Jail Time Records iyoanzishwa mwaka 2018.

Na tayari baadhi ya wafungwa wamesharekodi ngoma zao zinazofanya vizuri mitandaoni. Mmoja ya wafungwa hao ni Empereur. Ni kiongozi wa magenge ya uhalifu anayeogopwa ndani na hata nje ya gereza. Wimbo wake alirekodi video yote katika mazingira ya Gereza la New Bell na umetazamwa mara 24,000 kupitia YouTube.

Aidha, nyimbo za wasanii wenye vipaji vya muziki zimeweza kupenya na kufanya vizuri katika Afrika Kusini, Marekani na Argentina. Mapema mwaka huu (2026), Lebo ya Jail Time Records iliandaa na kufanikisha Tamasha kubwa la muziki la wafungwa wa Gereza hilo la New Bell.

“… Hapa tunachangia urafiki, upendo na sauti zinaweza kusikika,” anasema Steve Happi, mfungwa wa zamani wa Gereza hilo, ambaye pia ni sehemu ya waasisi wa Lebo ya Jail Time Records.

Kwa mujibu wa Happi, lengo la kuanzishwa kwa Lebo hiyo ni kuwaondoshea wafungwa msongo wa mawazo na kutokufikiria ugumu wa maisha ya gerezani. Mwonekano wa studio ya Lebo hiyo ni chumba kidogo kilichotenganishwa na kingine cha kuingiza sauti (booth), na kompyuta ya mezani moja.

Prodyuza wa studio ni Stone, mwanajeshi wa zamani wa Cameroon, ambaye alihukumiwa kifungo cha miaka 10 gerezani baada ya kukutwa na bangi na silaha.

Mbali ya kurekodi muziki, pia chumba hicho kimekuwa kikitumika kwa bunifu mbalimbali, ikiwamo utengenezaji wa makala za sauti na video (documentary).

Wanayo filamu iliyoongozwa na Happi kwa kushirikiana na msanii wa Italia, Dione Roach, ambaye pia ni muasisi mwenzake wa Lebo hiyo, ilirekodiwa ndani ya Gereza la New Bell kwa miaka zaidi ya sita.

Katika filamu hiyo, yanazungumziwa maisha ya gerezani na wiki chache zilizopita ilinyakua tuzo tatu, ikiwamo ya Tamasha la Tribeca jijini New York, Marekani.

Mwaka 2022, Happi na Roach wakishirikisha wafungwa waliachia albamu yao ya ‘Jail Time Vol 1’. Nusu ya faida ya mauzo ya albamu yalikwenda kwa wasanii na sehemu iliyobaki iliingia kwenye Lebo hiyo.

Related articles

Recent articles